WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua Mkutano Mkuu wa 11 wa
Kitaaluma wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA)
ambapo amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka wazingatie miiko ya taaluma yao
hususan utunzaji siri za Serikali na kufuata utaratibu rasmi wa utoaji taarifa.
“Hakikisheni mnadhibiti matukio yanayokiuka taratibu ikiwemo
kutumia mifumo rasmi katika kusafirisha na kutuma nyaraka badala ya kutumia
njia zisizo sahihi. Ninasisitiza kila mmoja azingatie wajibu wa kutunza nyaraka na kudhibiti utupaji ovyo wa
nyaraka na kusababisha kukutwa sokoni zikifungiwa bidhaa au kuachwa zikizagaa
na kukutwa katika mikono isiyo sahihi.”
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Oktoba 27, 2023, wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa TRAMPA katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete
jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza wadhibiti uvujaji wa
siri za Serikali.
“Wanachama wa TRAMPA zingatieni misingi ya kuanzishwa chama
chenu. Hiki ni chombo kinachowakilisha taaluma kwenye taasisi mbalimbali nchini
na siyo chama cha kisiasa hivyo fanyeni yaliyo ya kitaaluma kama alivyowaasa
Mlezi wa Chama chenu ambaye anataka kuona chama kikiendelea vizuri,” alisema
Majaliwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kila mtunza kumbukumbu awe
msaada na mlinzi wa mwenzake ili kudhibiti upotevu wa nyaraka na majalada yenye
taarifa muhimu. “Toeni taarifa kwa mamlaka kuhusu uwepo wa viashiria vya baadhi
ya maafisa kumbukumbu wasio na maadili wanaosababisha upotevu wa nyaraka.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma iweke mpango mahsusi wa kupunguza uhaba wa
watunza kumbukumbu ikiwa ni pamoja na kuandaa kanzidata, wabainishe mahitaji na
kuharakisha utoaji wa vibali vya ajira ya kada za watunza kumbukumbu kwa idara ambazo
tayari zimeshatenga ikama ya watumishi wa kada hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Maafisa Masuhuli
wasimamie Ofisi za Masijala kwa
kudhibiti vitendo vya kufanya ofisi hizo kuwa dampo au sehemu ya chakula. “Kila
Afisa Masuhuli asimamie vizuri taratibu za kutunza au kuhifadhi nyaraka. Pia
yapo mazoea ya baadhi ya Viongozi kuzifanya Ofisi za Masijala kutumika kwa kula
chakula. Ofisi ziwe na maeneo ya chakula.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa
ikifanya jitihada za makusudi kuimarisha sekta ya umma kwa kufanya maboresho
mbalimbali ili kuiwezesha sekta hiyo ikidhi matarajio ya umma. “Jitihada zote hizo haziwezi kuwa na manufaa
iwapo hakuna mifumo madhubuti ya kuhifadhi taarifa.”
Ametaja maboresho mengine kuwa ni pamoja na kuziboresha
masijala za Serikali kwa kuziwekea vifaa na vitendea kazi vyenye viwango ili
kukidhi mahitaji ya sasa kuharakisha utoaji huduma kwa wadau na wananchi kwa
ujumla na kutambua, kukusanya na
kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka muhimu katika kuhifadhi historia na urithi andishi
wa nchi yetu kwa matumizi ya sasa na kwa vizazi vijavyo.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni