Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora Mhe.Ridhiwani Kikwete (Mb) amewatahadharisha Watumishi wa Umma
kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la " Kausha
Damu" huku akisisitiza kuwa mikopo ya aina hiyo imekuwa ikidhalilisha na
kutweza utu wa Watumishi katika Jamii.
Mhe. Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na
Watumishi wa Halmashauri ya Busega Mkoani Simiyu wakati akihitimisha ziara yake
aliyoianza mapema wiki hii Mkoani Mara.
Amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya watumishi wa umma kuathirika
kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri utoaji
wa huduma bora kwa wananchi.
Amefafanua kuwa mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye
Taasisi za Kifedha zisizotambulika imekuwa na riba kubwa ambayo huwapelekea
Watumishi wengi kushindwa kuwasilisha marejesho na hivyo kupelekea kuuzwa kwa
nyumba au vitu vya thamani wanavyo vimiliki.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kikwete amewataka Watumishi kuanza
kutumia Mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans) ulioanza kutumika
kuanzia Septemba 1, 2023 ambao unamuwezesha Mtumishi wa Umma kuomba mkopo
pasipo kufika kwenye Taasisi ya Kifedha au Tawi la Benki.
Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais - UTUMISHI na
Utawala Bora ili kumsaidia Mtumishi wa Umma kupata mikopo katika Taasisi za
Kifedha zinazotambulika na Mwajiri ili kumuepusha Mtumishi kukopa sehemu ambazo
humpeleka Mtumishi kunyang'anywa kadi ya Benki.
Aidha, Mhe.Kikwete amewataka watumishi hao kujenga nidhamu
ya matumizi ya pesa wanazopata kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya baadaye
baada ya kustaafu.
Amewasihi kujiwekea malengo ya kujiandaa kustaafu kuanzia
leo ili wasije kuwa wateja wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na
Mfuko wa Kuendeleza Jamii (TASAF)
"Hakikisheni hata hela mnazozikopa mnafanya uwekezaji
wa kimkakati kwa ajili ya kujitegemea kiuchumi katika siku za mbeleni,"
amesisitiza Mhe.Kikwete.
Katika ziara hiyo Mhe.Kikwete mbali ya kuzungumza na
watumishi wa umma katika mikoa ya Mara na Simiyu pia amekagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na TASAF pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF.
Na. Lusungu Helela- Simiyu
0 Maoni