Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kufanya
upasuaji wa kwanza wa kifua kwa mgonjwa ili kuondoa uvimbe kwenye pafu kutumia
tundu dogo moja uliowashirikisha watalaamu wazalendo ukiongozwa na Bingwa wa
Upasuaji Kifua Duniani na mgunduzi wa upasuaji wa aina hiyo, Dkt. Diego Gonzalez Rivas kutoka nchini Hispania.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji (MNH) Dkt. Rachel Mhaville
amesema, upasuaji huu ni mwendelezo wa azma ya Serikali chini ya Wizara ya Afya
kuhakikisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinatolewa nchini na kuleta
unafuu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla ambao pia unaifanya Tanzania kuwa
nchi ya kwanza kutumia tundu moja dogo kupitia Hospitali ya umma katika Ukanda
wa Afrika Mashariki na Kati ukilinganisha na matundu matatu yaliyozoeleka
sehemu nyingine duniani.
Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili
Upanga Dkt. Ibrahim Mkoma amesema mgonjwa akifanyiwa upasuaji huo ambao siyo wa
kufungua kifua anaweza asihitaji kukaa ICU kama wagonjwa wengine wa upasuaji wa
kawaida na akaruhusiwa siku ya pili au ya tatu yake na kuendelea shughuli zake
za kawaida.
Dkt. Mkoma amesema wagonjwa wapatao wanne wanategemewa
kufanyiwa upasuaji wa aina hiyo na mara baada ya hapo watalaamu wazalendo
wataendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali.
0 Maoni