Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi
kuhusiana na taarifa zilizoenea mitandaoni kuhusu kufungiwa kwa Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro aliyehamishiwa hivi karibuni na
rais kushika wadhifa huo.
Taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Ofisa Habari na
Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, imesema kwamba usahihi ni kuwa Waziri Dk.
Ndumbaro alifungiwa miaka saba na uongozi wa TFF uliopita.
Ndimbo amesema kwamba hata hivyo, Dk. Ndumbaro hakukubaliana
na uamuzi huo, ambapo alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF
kupinga adhabu hiyo.
Amesema kwamba, Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF chini ya
uongozi wa sasa ilisikiliza rufani hiyo mwaka 2017, ambapo Waziri Ndumbaro
alishinda, na kuondolewa adhabu ya kufungiwa.
Katika taarifa hiyo, Ndimbo amemalizia kwa kusema kwamba kwa
sasa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro, ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Rufani ya Leseni ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
0 Maoni