Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imekanusha taarifa zinazosambazwa
kuhusu madai ya usafirishaji wa wanyamapori nje ya nchi kupitia maeneo ya
Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti.
Katika taarifa yake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusianao kwa Umma
wa mamlaka hiyo Joyce Mgaya amesema kwamba taarifa zinazosambazwa kupitia
baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu usafirishaji wa wanyamapori kwa kutumia
ndege za mizigo sio za kweli.
Aidha, amesema kwamba wawekezaji wote waliopo katika eneo la
Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Pololeti, wakiwemo kutoka Falme za
Kiarabu (UAE) na Marekani huendesha shughuli zao za utalii wa picha na uwindaji
kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Ikumbukwe kwamba eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni moja
ya maeneo ya Urithi wa Dunia chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO), na hutazamwa na taasisi zote ndani na nje ya
nchi ambazo husimamia shughuli za uhifadhi kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu," amesema Joyce.
Bi. Joyce amesema kwamba kutokana na sifa hizo, maeneo hayo
ya hifadhi hayajawahi kuwa maeneo ya kusafirisha wanyamapori wala kukiuka
misingi ya shughuli za uhifadhi wa rasilimali hizo za taifa.
Amemalizia taarifa yake hiyo kwa kuwaomba wananchi wapuuze
taarifa hizo, kwani sio za kweli na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea
kutekeleza majukumu yake ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
0 Maoni