Rais Samia azitaka nchi za Afrika kujiunga na Umoja wa Posta Afrika

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi za bara la Afrika kujiunga na Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ili zishirikiane kupiga hatua za maendeleo kwa kutumia huduma za posta kwa njia ya kidigitali.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jijiji Arusha, wakati akifungua jengo la kisasa la Umoja wa Posta Afrika ambapo amesema amearifiwa kuwa kuna baadhi ya nchi za Afrika bado hazijajiunga na umoja wa PAPU na zingine zinadaiwa ada za uanachama.

“Nilipokuwa napita kukagua jengo niliarifiwa kwamba kunabaadhi ya nchi za Afrika bado hazijajiunga na umoja huu, ni nchi 45 tu ndio zimejiunga na PAPU na baadhi yao hazijalipa ada za uanachama kwa muda, “alisema Rais Samia na kuongeza, “Nazisihi nchi za Afrika kujiunga PAPU na kwa zile ambazo hazijalipa ada zao zifanye malipo yao ili twende pamoja katika maendeleo ya huduma za posta”.

Rais Samia ametumia ufunguzi huo kuhimiza kuwa ili kwenda pamoja kwa mafanikio, jengo hilo la PAPU linapaswa kujenga uwiano wa utoaji wa huduma zake kwa usawa katika mataifa yote ya Afrika na kuchangia kuleta maendeleo.

Rais Samia pia amezipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa kusimamia na kukamilisha ujenzi wa jengo hilo refu na la kisasa Jijini Arusha na ambalo pia ni kivutio cha utalii.

Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Posta Duniani Bw. Masahiko Metoki ambaye alishiriki uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo hilo 2020, ameipongeza serikali ya Rais Samia kwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo PAPU litakaloendeleza huduma za posta Afrika.

Naye Katibu Mkuu wa PAPU Sifundo Chief Moyo, amesema kwamba jengo hilo la umoja huo la kihistoria limejengwa kwa fedha za nchi za Afrika hadi kukamilika kwake bila kutegemea wafadhili ambapo asilimia 60 ya gharama zimebebwa na PAPU na asilimia 40 na Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) leo Jijini Arusha akishirikiana na Katibu Mkuu wa PAPU Sifundo Chief Moyo. Ujenzi wa jengo hilo la ghorofa 17 umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 54.

Chapisha Maoni

0 Maoni