Tanzania kuanza kuzalisha kwa mara ya kwanza dawa ya kuulia
wadudu isiyokuwa na sumu katika kiwanda cha Viuadudu cha Tanzania Biotech Products
Limited kilichopo Kibaha katika mkoa wa Pwani kinachomilikiwa na Shirika la
Maendeleo ya Taifa (NDC).
Akiongea katika video fupi aliyoituma kutoka Jijini Havana, Balozi
wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amesema tayari wameshampata
mtaalamu bingwa na mbobezi kutoka Cuba na wiki ijayo atakuja nchini kwa ajili
ya kazi hiyo.
“Tayari tumeshapitia nyaraka zake na wiki ijayo mimi
mwenyewe nitamsindikiza uwanja wa ndege kuhakikisha anakuja nyumbani kwetu Tanzania,
na huyu ni mtaalamu tutamuweka katika kiwanda chetu cha kutengeneza viuadudu
pale Kibaha kwa ajili ya kuzalisha dawa hiyo,” alisema Balozi Polepole.
Amesema kwa sasa, uzoefu ni kwamba tunapulizia sumu ili kuua
wadudu wanaoshambulia mazao katika mahindi, maharage, pamba na aina zote za
mazao, ila sasa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania itaanza uzalishaji wa dawa
ya kuua wadudu isiyo na sumu aina ya Bio Pesticides.
“Zama za kupulizia sumu kuulia wadudu kupata magonjwa ya
kansa na magonjwa ya ngozi na kila kitu zimekwisha, tutumie dawa hii ya kuulia
wadudu wanaoharibu mazao ambayo sio sumu,” alisema Balozi Polepole na kuongeza “Dawa
hii imethibitika na cheti imeshapata kutoka Tanzania inatambulika na inafanya vizuri
zaidi kuliko dawa zenye sumu, achana na sumu tumia Bio Pesticides, tunataka
kuanza katika msimu huu afya kwa Watanzania. “
0 Maoni