MSD kuongeza nchi mbili za SADC manunuzi ya dawa kwa pamoja

 

Bohari ya Dawa (MSD) inakamilisha mchakato wa kuingiza mahitaji ya nchi mbili za Zambia na Malawi katika mpango wa manunuzi ya dawa kwa pamoja kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Hayo yamelezwa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Ali Tukai, alipokuwa akiongea na Wahariri wa vyombo vya habari wakati akielezea mafanikio ya Bohari ya Dawa, ambapo kwa sasa chini ya mpango huo wanazihudumia nchi mbili za Comoro na Seychelles.

“Kwa sasa tunahudumia nchi za Comoro na Seychelles chini ya mpango wa manunuzi ya dawa kwa pamoja kwa nchi za SADC, pia mahitaji ya nchi za Zambi na Malawi yapo katika ukamilishaji ili kuanza kuhudumiwa,” alisema Bw. Tukai na kuongeza kuwa, “Changamoto inayoukabili mpango huo wa manunuzi ya dawa wa pamoja kwa nchi za SADC, ni kutokana na ushiriki wake kuwa wa hiari.”

Ameeleza hatua zinazochukuliwa ili kuongea ufanisi wa mpango huo kuwa ni kuboresha ushirikiano na kuongeza ushawishi katika ngazi ya SADC Sekretarieti, na katika ngazi ya Nchi za SADC kupitia balozi zetu. Pia kushirikisha viwanda vilivyopo nchi za SADC kwenye mpango wa ununuzi wa pamoja.

Kuhusu kuimarika kwa upatikanaji wa bidhaa za afya, Bw. Tukai amesema upatikanaji wa bidhaa za afya umeongezeka kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 Juni 2023, huku upatikanaji wa dawa ukifikia asilimia 81 mwezi Juni 2023 kutoka asilimia 57 mwezi Juni 2022.

Pia, Bw. Tukai amesema Serikali imeongeza fedha za ununuzi wa bidhaa za afya ambapo fedha iliyopokelewa mwaka wa fedha 2022/23 ni sh bilioni 190.3 ikilinganishwa na sh bilioni 134.9 mwaka wa fedha 2021/22, sawa na asilimia 95.

Chapisha Maoni

0 Maoni