Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni mambo muhimu
kwa nchi zinazoendelea hasa katika masuala ya uchumi wa kijamii kwa vile nchi
hizo zinaweza kubadili maisha ya watu wake kupitia sekta muhimu kama ya kilimo,
nishati na elimu.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipohutubia katika Mkutano
wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Kundi la 77 pamoja na China akimwakilisha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unaofanyika
katika ukumbi wa mkutano, Havana Cuba.
Aidha Mhe. Dk. Mwinyi amekumbusha namna nchi zinazoendelea
zilivyoathirika vibaya na janga la maradhi ya UVIKO-19, kwa kupanda kwa bidhaa, mizozo ya kisiasa na athari
zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema hizo ni baadhi ya changamoto zilizosababisha kupanda
kwa gharama za maisha na kudhoofisha jitahada za kujikwamua kiuchumi kwa nchi
zinazoendelea.
Katika hotuba yake alikumbushia namna nchi zilizoendelea
zilivyobaniwa teknolojia ya kutengeneza chanjo nchi za mataifa ya kusini na
kuzinyima kabisa msaada wa kiteknolojia ili ziweze kutengeneza chanjo, hali
hiyo iliyosababisha makampuni ya utengenezaji dawa ya mataifa tajiri kujipatia
faida kubwa kwa kuziuzia nchi masikini chanjo ya UVIKO-19.
Rais Dk Hussein Ali Mwinyi akazitanabahisha nchi za kundi la
G77 na China wachukulie hayo yote kama somo na zisibweteke kusubiri msaada kutoka
mataifa tajiri, huu ndio wakati wa kusema imetosha.
📍Havana, Cuba.
0 Maoni