Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inatambua fursa zilizopo katika Kilimo Hai
kupitia mkakati uliondaliwa na Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na wadau
utakuwa ni suluhisho kwa changamoto za sekta ya Kilimo Hai ikiwemo upatikanaji
wa pembejeo za kibaolojia, elimu kwa wakulima na wafugaji pamoja na upatikanaji
wa masoko ya ndani na nje ya nchi ya bidhaa zinatokana na Kilimo Hai.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo jana wakati akifungua Tamasha
la Kilimo Hai na kutembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya Dole
Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza matumaini yake kupitia
mkakati uliondaliwa na Serikali kuwa utatengeneza programu madhubuti ya utekelezaji
ya kuwapa fursa vijana kwa kuanzisha biashara za kutengeneza viatilifu na
mbolea hai ili kusaidia upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi na
kuitangaza Zanzibar kuwa kivutio cha kijani na kuendana na utalii endelevu.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi ametoa wito katika utoaji wa
elimu kwa watumiaji na walaji kuzifahamu faida za Kilimo Hai kuepusha chakula kinachozalishwa
kupitia matumizi ya kemikali ili kupunguza maradhi yasiyoyambukiza ikiwemo
saratani, shinikizo la damu na kisukari.
0 Maoni