WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa madhehebu
ya mbalimbali ya dini nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kupiga
vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
"Tushirikiane kupambana na biashara na matumizi ya dawa
za kulevya ambayo yameathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa,"
alisema Majaliwa.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba
28, 2023), alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
Baraza la Maulid lililofanyika Kitaifa jijini Dodoma kwenye kituo cha Mikutano
cha Jakaya Kikwete.
“Matumizi ya dawa za kulevya yana madhara mengi kwa Taifa
yakiwemo ya kiuchumi, kiafya na kimazingira pamoja na kuathiri uwezo wa mtu
kufikiri,” alisema Majaliwa.
Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini waendelee
kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii na wawahamasishe waumini
kushiriki katika shughuli zitakazowaongezea kipato.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waendelee
kudumisha amani nchini kwa kuwa amani ni jambo la msingi katika maendeleo ya
Taifa. "Tuendelee kuishi kwa amani na upendo pamoja na kuliombea dua Taifa
na viongozi wakuu. "
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo
kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote
watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya
madaraka, hivyo waendelee kuiamini Serikali yao.
Awali, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
Alhaj Nuhu Jabir Mruma amesema kuwa Baraza hizo linaridhishwa na utendaji kazi
wa Rais Dkt. Samia za kuwaletea watanzania maendeleo katika Sekta za Uchumi,
Siasa, Kijamii pamoja na kuboresha mfumo wa demokrasia nchini.
Aidha, Alhaj Mruma ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali
iongeze wigo wa kutoa elimu ya uraia kwa kushirikiana na viongozi wa dini ili
kuwawezesha wananchi kupata uelewa na washiriki katika chaguzi zijazo ukiwemo
wa Serikali za Mitaa inayotarajiwa kufanyika 2024.
0 Maoni