Rais Dk. Mwinyi asema uchumi wa Zanzibar una fursa nyingi za masoko

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imejizatiti kutimiza ahadi na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025 ya kuzalisha fursa mbalimbali za ajira ikiwemo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na wajibu wa Serikali kuandaa mazingira wezeshi ili kuinua fursa hizo.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 25 Septemba 2025 wakati akifungua Tamasha la kwanza la Fahari ya Zanzibar na mwaka mmoja wa Taasisi ya Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeendelea na hatua za kuimarisha miundombinu ya mazingira ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali ikiwemo ujenzi wa masoko na vituo vya mabasi.

Vilevile, amesema uchumi wa Zanzibar una fursa nyingi za masoko kwa kuwepo kwa hoteli nyingi za kitalii kwa mahitaji ya bidhaa mbalimbali hivyo amewataka wadau wanaojihusisha na sekta ya utalii kuhakikisha wajasiriamali wazawa wananufaika na fursa hizo.

Halidhalika Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wajasiriamali hao kuzalisha bidhaa kwa viwango vinavyohitajika ili kupunguza uingizaji wa bidhaa za nje ili kuimarisha soko la ndani.

Chapisha Maoni

0 Maoni