Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) imefanya
semina elekezi kwa Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, mkoani Arusha.
Aidha, semina hiyo iliyofanyika jana ililenga kutoa uelewa kwa Kamati hiyo
kuhusu majukumu yanayotekelezwa na OSHA na namna taasisi hiyo iliyopo chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu inavyosimamia masuala ya Usalama na Afya katika sehemu za
kazi.
Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi
wa mafunzo hayo, amesema masuala ya usalama na afya ni mtambuka na yanagusa
sekta zote za uchumi, hivyo ni vyema kushirikiana kuimarisha mifumo ya usimamizi
wa usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Sillo Baran
(MB), ameishukuru OSHA kwa mafunzo hayo ambayo yamewajengea uelewa mzuri kuhusu
masuala ya usalama na afya. Pia ameitaka OSHA kuendelea kutoa elimu hiyo kwa
wafanyakazi nchini ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.
Akizungumza awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru kamati
hiyo kwa kuishauri vyema serikali kuhusu masuala ya usimamizi wa usalama na
afya mahali pa kazi na amewahakikishia ofisi hiyo itaendelea kusimamia kwa
ufanisi masuala hayo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa
Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema taasisi hiyo itahakikisha ustawi
wafanyakazi unaimarika sambamba na kulinda uwekezaji kupitia mifumo ya usalama
na afya.
Na. Mwandishi Wetu- Arusha
0 Maoni