Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Tri Yogo Jatmiko
amesisitiza kushirikiana na Tanzania katika kutangaza Mwelekeo Mpya wa Wizara
wa VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri ili kutangaza fursa mbalimbali za
uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini Nchini.
Balozi Jatmiko amesema hayo jana jijini Dodoma mara baada ya
mazungumzo mafupi na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali katika kikao
kilicholenga kujenga mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika shughuli za
uchimbaji madini
“Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimbali mbalimbali za
madini ambazo ni muhimu na zinahitajika duniani. Kupitia Dira hiyo Sekta ya
Madini inakwenda kutangaza nchini Indonesia na kueleza wawekezaji fursa
mbalimbali zilizopo,” amesema Mhe. Jatmiko.
Ameongeza kuwa, kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya
nishati hiyo hususan magari ya umeme katika nchi hiyo, Serikali ya Indonesia
itaweka vipaumbele katika matumizi ya madini mkakati kutoka nchini Tanzania ili
waweze kukidhi mahitaji yao katika matumizi mbalimbali ya vifaa vya umeme.
Katika hatua nyingine, amempongeza Waziri wa Madini Mhe.
Antony Mavunde kwa kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa
Waziri wa Madini. Amesema nchi hiyo itatoa ushirikiano wa kutosha nchini ili
kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri
Mahimbali amesisitiza nchi hiyo kutoa ushirikiano katika kuwajengea uwezo
wataalam mbalimbali wa wizara na taasisi katika maeneo ambayo yatahitajika
ikiwemo mafunzo ya Uongezaji Thamani Madini na mafunzo maalum kwa wakufunzi
wachache ambao watakuwa walimu katika kutoa mafunzo maeneo muhimu.
Pia, ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika
Sekta ya Madini ikiwemo ushirikiano katika uchimbaji wa madini ya dhahabu na
madini ya kimkakati. ‘’Tunahitaji ushirikiano katika maeneo ya uchimbaji wa
madini hayo kupitia Shirika la Madini la Taifa STAMICO na sisi Serikali tutatoa
ushirikiano ili uchimbaji wa madini hayo ufanyike hapa nchini,” amesema
Mahimbali.
Vile vile, amewakaribisha kushiriki katika Jukwaa la
Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini linalotarajiwa kufanyika Oktoba
25 na 26 mwaka huu. Amesema jukwaa hilo litatangaza fursa mbalimbali za
uwekezaji zilizopo nchini.
Kikao hicho kifupi kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga pamoja na
wataalam mbalimbali wa Wizara.

0 Maoni