Jela miaka sita kwa kuvunja Ofisi ya Mganga Mkuu na kuiba pikipiki

 

Watu wawili akiwemo raia wa Burundi Niyokindi Anthony (44), wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka sita gerezani baada ya kukiri kutenda kosa la kuvunja Ofisi ya Mganga Mkuu wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza na kuiba pikipiki tatu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi na moja huku mmoja akikana shtaka na kurudishwa rumande kwa kukosa dhamana

Mbali na raia wa Burundi mwingine aliyehukumiwa kutumikia kifungo hicho ni mkazi wa Isungangh'olo wilayani Sengerema Ibrahim Mshengezi (55) ambapo wamehukumiwa kwa kutenda makosa mawili ambayo ni kuvunja ofisi na kuiba kinyume na vifungu 297 na 258 vya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kesi hiyo yenye washtakiwa watatu, mshtakiwa mwingine ambaye ni Mkazi wa Isungangh'olo wilayani Sengerema, Anold Paul (25) amekana mashtaka hayo ambapo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Evod Kisoka ameamuru arejeshwe rumande baada ya kukosa wadhamini

Awali, akiwasomea maelezo ya kosa washtakiwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sajenti wa Polisi Theophilius Bei alisema washtakiwa walitenda makosa hayo Agosti 20 mwaka huu kwa kuiba pikipiki tatu za Serikali zenye namba ya usajili, SM15342, SM15343 na SM15349, zote kampuni ya Yamaha kinyume na Kanuni ya adhabu Sura ya 16 toleo la mwaka 2022.

Hata hivyo, shtaka dhidi ya mshtakiwa namba tatu (Anold Paul) ambaye amekana mashtaka hayo litaendelea tarehe 2/10/2023.

Hakimu Kisoka amesema Mahakama inatoa hukumu ya miaka sita kwa washtakiwa ili iwe funzo kwa wengine.

CHANZO: Mimi Online Tv

Chapisha Maoni

0 Maoni