EWURA yavifungia vituo viwili kwa kuhodhi mafuta

 

EWURA imevifungia vituo vingine viwili vya mafuta kwa kosa la kuhodhi mafuta, kati ya mwezi Julai na Agosti 2023, Vituo hivyo ni Rashal Petroleum Ltd-Mlimba, Mkoa wa Morogoro na Kimashuku Investment Co. Ltd-Babati, Mkoa wa Manyara.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Tarehe 30/09/2023, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA Bw. Titus Kaguo amesema: “Kila tunapokifungia kituo kwa miezi sita tunataka umma ufahamu kwa sababu hawa ndio wanaochangia kusuasua kwa usambazaji wa mafuta hapa nchini.”

Aidha, Bw. Kaguo alisema pamoja na mafuta kuwepo nchini, changamoto ya upungufu wa mafuta katika maeneo mbalimbali ilichangiwa na baadhi ya wamiliki wa vituo kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi ya kibiashara, ikiwemo faida kubwa kutokana na ongezeko la bei za mafuta kinyume na sheria.

EWURA imetoa onyo kali kwa wauzaji wa Jumla na wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa Serikali inafuatilia suala hilo kwa karibu kupitia vyombo vyake mbalimbali na ikithibitika uvunjaji wa sheria na kanuni umetendeka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafutia leseni zao za biashara.

Chapisha Maoni

0 Maoni