Mkazi Kata ya Mkindi, wilayani Kilindi; mkoani Tanga, Tabu
Mokiwa, amekatwa mkono huku mtoto wake akijeruhiwa kichwani, baada ya kudaiwa
kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.
Akizungumzia tukio hilo, mtoto Halima Shabani, amesema
walivamiwa na watu usiku, ambao wanadhani ni wafugaji ambao inadaiwa
walimshambulia mama yake hadi kumkata mkono, na kwamba alipojaribu kumsaidia,
naye alikatwa mara tatu kichwani.
Amesema watu hao walianza kwa kupiga hodi na mama yake
kuuliza ni wakina nani, ila watuhumiwa hao walilazimisha mlango ufunguliwe, na
kwamba familia hiyo ilipogoma, ndipo watuhumiwa wanadaiwa kuvunja mlango huo.
Mtoto huyo ameongeza kuwa baada ya kuvunja mlango
walimuuliza mama yake kuwa kama yeye ndiye Tabu na alipojibu kuwa niyo yeye,
inasemekana watu hao walianza kumshambulia mama huyo kwa kumkata na vitu
vinavyosadikiwa kuwa nan cha kali.
"Mama wamemkata mkono kabisa nilipoona wanazidisha
nilimsaidia, lakini na mimi nilikatwa kichwani na mkononi, wote tumeumia sana,
ila mama kapoteza mkono wake,” amesema Halima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe,
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa analifuatilia kupata
taarifa zaidi kwani yupo safarini na kwamba atatoa taarifa kamili kuhusu tukio
hilo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Handeni, Hudi Shehdadi,
amekiri kupokea majeruhi wawili wa tukio hilo na kwamba wanaendelea na matibabu
hospitalini hapo.
Naye mkazi wa Kata ya Mkindi, Rajabu Lukuwa, amesema kwa
sasa hawana amani na kwamba wanaishi kwa hofu kutokana na matukio kama hayo.
Kwa maelezo ya majeruhi hao, chanzo cha ugomvi huo ni
mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kata ya Mkindi.
CHANZO: Gazeti la Mwananchi.
0 Maoni