Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema mazingira mazuri ya
uwekezaji yaliyowekwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sekta binafsi
yamechochea ukuaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Aidha, Mhe. Ndalichako amesema ukuaji huo umepelekea thamani
ya mfuko kuongezeka pamoja na michango ya wanachama.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo jana alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya NSSF kwa mwaka 2022/23 kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii.
Amesema kwa mwaka 2022 mfuko huo uliandikisha wanachama
233,644 hadi kufikia Juni mwaka 2023 kulikuwa na wanachama 243,895 na matarajio
ifikapo Juni 2024 ni kuwa na wanachama 277,279.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq,
ameutaka mfuko wa NSSF kuhakikisha unaongeza wanachama zaidi hasa waliopo
kwenye sekta isiyo rasmi.
Akijibu hoja za wabunge, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha
Mshomba, amewahakikishia wabunge kuzingatia maoni yao ili kuendelea kuboresha
huduma kwa wanachama wake.
0 Maoni