Kampuni ya Twiga Minerals Cooperation Limited inayomilikiwa
kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick
Gold Cooperation imeongoza katika kipengele cha Kampuni zenye ubia na Serikali
katika utoaji Gawio kwa Serikali.
Tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ilitolewa Agosti 19, 2023
jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu
na Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa
kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma.
Akizitaja kampuni zilizofanya vizuri katika kipengele hicho,
Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema kuwa kampuni ya Twiga imefanya vizuri
katika kipengele hicho kwa kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi
bilioni 84 Mwaka wa Fedha 2022/23.
Kampuni ya Barrick ndiyo kampuni ya kwanza kuingia ubia na
Serikali miongoni mwa kampuni za madini hali ambayo ilihamasisha na kampuni
nyingine kutoka nje kusaini mikataba yenye thamani kubwa na Serikali katika
shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbaimbali yakiwemo madini muhimu na ya
mkakati.
Aidha, ubia na kampuni hiyo umetajwa mara kadhaa kuwa mfano
wa kuigwa na mataifa mbalimbali huku kampuni hiyo ikitaja kuutumia ubia wa Tanzania
kuutekeleza katika nchi nyingine ilikowekeza.
Migodi iliyo chini ya kampuni ya Twiga Minerals ni pamoja na
North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi.
Mwezi Januari, 2023 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja Mkazi wa kampuni ya Twiga
Melkiory Ngido alisema mwaka 2020 kampuni hiyo ilitoa gawio kwa Serikali kiasi
cha Dola za Marekani milioni 250 huku kipindi cha mwaka 2017 hadi 2022 kiasi
cha shilingi bilioni 24.3 kilitolewa kwa halmashauri kama tozo mbalimbali
zinazotozwa katika maeneo yenye shughuli za migodi yake.
" Kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa
migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu na ni matazamio ya uhai wa mgodi wa
Bulyanhulu ni kufika mwaka 2040 na North Mara kufika mwaka 2039,"
alisema Ngido katika kikao hicho.
0 Maoni