Polisi yatoa onyo: Ole wake atakayeshiriki maandamano

 

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camilius Wambura ametoa onyo kali kwa kundi la watu waliosambaza taarifa kuwa wanaandaa maandamano nchi nzima juu ya kuiangusha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kabla ya mwaka 2025.

IGP Wambura ametoa onyo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, na kusema cha ajabu wamehusisha maandamano hayo wanayoyapanga kushawishi Watanzania kuwaunga mkono na hoja zinazoendelea za mjadala wa bandari.

"Sisi tuliamini suala la bandari linajibiwa kwa hoja na na vilevile tukaamini kwa sababu hawa watu walikwenda mahakamani wangeheshimu maamuzi ya Mahakama lakini badala yake wametoka sasa na kuanza kutafuta ushawishi na kuwataka Watanzania waingie kwenye maandamano ya nchi nzima na miongoni mwao mmoja amekwenda mbali zaidi na kusema watahakikisha wanaangusha Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya awamu ya sita," amesema IGP Wambura.

IGP Wambura amewasisitizia kwa kuwaonya vikali wasitishe kabisa matamshi yao hayo ya kichochezi kwa kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa uhaini wanaotaka kuufanya kwani yote ni makosa ya jinai na Jeshi la Polisi halitakaa kimya na kuwavumilia hicho wanachotaka kukifanya na kuvunja amani iliyopo.

"Kama mfikiria tupo kimya basi tutakwenda kuwaonyesha hatuko kimya kwa yeyote anayevunja sheria ya nchi hivyo niwatake Watanzania wawapuuze watu hawa kwani Tanzania ni nchi ya amani na salama hawa wasitake kuwashawishi na kuingiza nchi kwenye machafuko hatujawahi kufika huko na hatutofika kwenye machafuko, " amesema IGP Wambura.

Aidha, wachochezi hao wametakiwa kutambua kuwa Jeshi la polisi ni imara sana wasitikise kiberiti kama waliwahi miaka ya huko nyuma na wakaguswa wasithubutu kwenda hatua nyingine huko wanakoshawishi kwenda ni sehemu mbaya sana hivyo wananchi muwe watulivu muendelee kuishi kwa amani mkiendelea kufanya shughuli zenu za kiuchumi kama ilivyokuwa desturi yenu.

CHANZO: UMG digital

Chapisha Maoni

0 Maoni