Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kunadi vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi mbalimbali wanaotembellea banda la NCAA katika viwanja vya John Mwakangale Mbeya, Nzuguni - Dodoma na viwanja vya Themi Jijini Arusha.
Afisa Uhifadhi Mkuu kitengo cha Uhusiano wa Umma, Joyce
Mgaya amebainisha kuwa katika maonesho hayo muamko wa wananchi kutembelea kwa
ajili ya kupata elimu umekuwa mkubwa na wengi wanahamasika kujipanga kwa
makundi kutembelea vivutio vya Utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Maonesho haya sehemu kubwa ni ya wakulima na wafugaji lakini
shughuli hizi zinachangiwa na matokeo ya Uhifadhi endelevu katika maeneo ya
misitu yaliyohifadhiwa ambayo ni vyanzo vya kuleta mvua na vyanzo vya maji
yanayotumika kwenye mashamba ya wananchi kwa ajili ya matumizi ya kilimo cha
umwagiliaji, ufugaji na maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu.”
Msimamizi wa Banda la NCAA Arusha ambae ni Afisa Utalii
Mwandamizi Zaynab Suleiman anabainisha kuwa hamasa ya wananchi kupata elimu ya
vivutio imekuwa kubwa na waliowengi wamehamasiska kupanga safari za kutembelea
eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hasa kupitia makundi mbalimbali kwa ajili kuwa na
safari za pamoja kutokea Arusha.
Kwa upande wake kiongozi banda la nanenane kanda ya Kati
Dodoma Afisa Uhifadhi Mkuu Lowaeli Damalu ameeleza kuwa katika juhudi za
kufikisha elimu ya uhifadhi na utalii kwa wadau wengi katika maonessho hayo
watumishi wa NCAA wanatembelea mabanda yote katika viwanja hivyo ili kuwafikia
watu wengi na kuongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi na utalii kwa washiriki wa
maonesho hayo.
Aidha, msimamizi wa Banda la NCAA katika viwanja vya John
Mwakangale Mbeya Afisa Uhifadhi Msaidizi Abdiel Laizer anabainisha kuwa katika
viwanja hivyo wananchi wameendelea kupata elimu ya uhifadhi na utalii hususan
wa mali kale katika kimondo cha Mbozi na makumbusho ya kimondo cha mbozi yenye
vielelezo vya tamaduni mbalimbali na kutaka kujua bei na utaratibu wa kufika
katika vivutio hivyo.
0 Maoni