Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu
Hassan, amesema kwamba Serikali haijafunga mipaka uuzaji mazao nje ya nchi,
bali ina lengo la kuwa na mfumo rasmi wa ununuzi, uuzaji na usambazaji wa mazao
utakaoweza kutambua kiasi cha mazao yanayouzwa nje ya nchi.
Akiongea leo kwenye sherehe za kilele cha Siku ya Nanenane
Jijini Mbeya, Mh. Samia amesema kwamba kwa hali ilivyo sasa Serikali haitambui
kiasi halisi cha chakula kinachouzwa nje kutokana na wanunuzi wa nje kwenda
moja kwa moja kwa wakulima na kununua mazao.
“Uzoefu uliopo sasa nikwamba magari yanatoka tu nchi jirani
yanaingia moja kwa moja kwenye mikoa yetu, moja kwa moja kwenye wilaya zetu
hayaulizwi yanakwenda mpaka kwa wakulima yananunua mazao na pale wanakwenda
kulipa fedha zetu na wala hatupati fedha za kigeni,” alisema Mh. Samia.
Tukiweka mfumo mzuri wa ununuaji, tukidhibiti magari
yanayokwenda moja kwa moja kununua kwa wakulima tutajua tunanunuaje na tunauzaje,
“Ndio maana mwaka huu nikakupa fedha nyingi Mheshimiwa Waziri Bashe ili NFRA inunue
mazao kwa wakulima tuyahifadhi ghalani ili watu wa nje waje kununua mazao hayo,
lakini hakuna mkulima kuuza mazao moja kwa moja”.
Pia, Rais Samia amesema Serikali imeendelea kufanya jitihada
za makusudi za kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo pamoja na wanawake,
miongoni mwa jitihada hizo ni kuanzishwa kwa programu ya miaka minane ya kilimo
inayojulikana kama Jenga Kesho iliyo Bora ama Bulding A Better Tomorrow (BBT).
“Hadi sasa vijana waliokidhi vigezo 812, wanawake 282 na
wanaume 530 wanaendelea na awamu ya kwanza ya mafunzo ya kilimo au kilimo
biashara katika vituo hatamizi 13 ambayo yanatolewa kwa miezi minne, baada ya hapo
watapatiwa mashamba yanafofikia hadi hekari 10 na yatakodishwa kwao kwa miaka
66,” alisema Rais Samia.
Katika kuhakikisha mbolea inamfikia mkulima kwa bei nafuu
hadi katika ngazi ya Kata, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Kilimo Mh. Hussein
Bashe kukutana na Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba kuona namna Serikali itakavyosaidia
kupunguza gharama za usafiri ili kutombebesha mzigo mkulima.
Rais Samia pia amekumbushia tena agizo lake alilolitoa mwaka
2022 siku kama ya leo la kutaka kufanyika maonesho ya kilimo katika mikoa yote
nchini ikiwa ni pamoja na kutenga viwanja vya maonesho ya Nanenane, ili
kuchochea kasi ya ukuaji wa kilimo nchini.
Kwa upande wake Waziri wa kilimo Mh. Husein Bashe
ameishukuru Serikali kwa kutoa ruzuku ya mbolea ambapo kwa mwaka huu serikali
itatoa zaidi ya shilingi bilioni 200 kama ruzuku na kuongeza kwamba matumizi ya
mbolea yataongezeka na kufikia tani 951000.
Kuhusu programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Bulding A Better
Tomorrow) Mh. Bashe amesema kwamba kwa mara ya kwanza vijana wakitanzania
watapatiwa umiliki wa ardhi, nyumba na mashamba kwa ajili ya kilimo na awamu ya
kwanza itakuwa tarehe 20/08/2023.
Mhe. Bashe pia ameonekana kukerwa na vitendo vya uvamizi wa
maeneo ya utafiti na mashamba ya mbegu na kuwataka wavamizi kuacha mara moja
kufanya hivyo kwani hakuna maendeleo ya kilimo yatakayoweza kufikiwa bila ya
uwepo wa mashamba ya mbegu.
Katika sherehe hizo Mh. Rais Samia Suluhu Hassan alitoa tuzo
kwa mikoa iliyoongoza kwa uzalishaji mazao ya nafaka ya Ruvuma, Rukwa na Mbeya
pamoja na ile ilioyoongoza kwa mazo yasiyo ya nafaka ya Kagera, Kigoma na
Mbeya.
0 Maoni