Naibu Katibu Mkuu Maliasili awapa kongole wahifadhi TANAPA

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba aipongeza TANAPA kwa juhudi mbalimbali inazozifanya katika kuhifadhi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo chini ya TANAPA.

Kamishna Wakulyamba, ametoa pongezi hizo leo tarehe 14.08.2023 wakati wa ziara ya Kikazi makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), jijini Arusha ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea TANAPA tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.

Awali, akimkaribisha Kamishna Wakulyamba katika kikao na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi kilichofanyika katika makao makuu ya TANAPA, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema alisema shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linatunza na kusimamia maeneo ya uhifadhi kwa niaba ya watanzania na kubainisha kuwa maeneo yanayosimamiwa ni muhimu kwas ajili ya uhifadhi na kubainisha kuwa maeneo haya ni vyanzo vikubwa vya maji ambayo yanasaidia uchumi wa nchi yetu katika maswala ya kilimo lakini pia upatikanaji wa umeme.

“Umuhimu wa Hifadhi ya Ruaha ni kwamba mtiririko wa mabwawa makuu matatu yanayozalisha umeme nchini vyanzo vyake vingi vinapatikana Hifadhi ya Taifa Ruaha ambayo ndio inatunza maji katika eneo la Ihefu lakini vyanzo vinatoka katika Hifadhi ya Taifa Kitulo na Mpanga Kipengere kuzalisha maji bwawa la Mtera, Kidatu na Nyerere.” alisema Kamishna Mwakilema.

Akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi TANAPA Makao Makuu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna Wakulyamba alibainisha majukumu mawili makubwa ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kusisitiza kutunzwa kwa Rasilimali hizi za Taifa kwa faida ya sasa na ya baadae.

“Sote tunafahamu majukumu ya Wizara hii ambayo jukumu la kwanza ni Uhifadhi lakini jukumu la pili linalozaliwa na Uhifadhi ni Biashara hapo ndipo linapokuja swala la Utalii na uvunaji wa Maliasili tulizonazo”.

Pia, Kamishna Wakulyamba aliipongeza TANAPA kwa utekelezaji wa miradi ya UVIKO -19 kwa ubora wa hali ya juu na kukamilika kwa wakati na kusisitiza utunzwaji wa miradi hiyo ili ilete faida iliyokusudiwa.

“Nimetembelea miradi ya UVIKO-19 TANAPA nimeona Ujenzi wa malango, ukarabati wa viwanja vya Ndege, Barabara na Nyumba za watumishi kwa kweli mmefanya kazi nzuri sana, niwatake miradi katika maeneo yale imetumia fedha nyingi hivyo tuitunze ili iendelee kuwa Bora na kile kilichokusudiwa na serikali tuweze kukipata kama ambayo tumeanza kukipata kwa kuongezeka idadi ya wageni katika maeneo yale” Alisema Kamishna Wakulyamba.

Vilevile Kamishna Wakulyamba aliwataka Maafisa na Askari wote wa Uhifadhi kudumisha misingi ya Jeshi kwa kuwa na Nidhamu na Uadilifu na kubainisha jeshi lolote duniani msingi wake mkubwa ni Nidhamu na Uadilifu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba yupo katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi iliyotekelezwa chini ya ufadhili wa fedha za ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya UVIKO -19 katika Kanda ya Kaskazini.

Na. Edmund Salaho- Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni