Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imesema kuwa itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuwekeza
katika kutekeleza miradi ya Sekta ya Nishati nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Maendeleo ya
Uchumi wa China, Liao Min wakati alipokutana na Waziri wa Nishati January
Makamba, Agosti 14, jijini Dar Es Salaam na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu
ushirikiano katika uwekezaji na uendelezaji wa miradi ya Sekta ya Nishati
inayofadhiliwa na China.
Katika mazungumzo yao, Min alimueleza Makamba kuwa nchi yake
itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya umeme kwa kuwa Tanzania
imekuwa ikitoa matokeo chanya katika kila miradi inayofadhiliwa na nchi hiyo,
hivyo kuifanya nchi hiyo kujenga uaminifu kwa Tanzania na kuendelea
kushirikiana katika sekta ya nishati.
Waziri huyo wa China alieleza kufurahishwa kwake na
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na kueleza kuwa mwezi Novemba mwaka
jana Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea nchi hiyo wakati wa sherehe za
kuadhimisha miaka 20 ya Chama cha Kimomunisti cha China.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati
Mbadala, Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, kwa niaba ya Katibu Mkuu,
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Decklan
Mhaiki, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Mhandisi Jones Olotu na Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji
Mafuta na Gesi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kenneth
Mutaonga.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba
ameishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika
kutekeleza miradi mikubwa katika sekta ya Miundombinu ya usafiri na Nishati kwa
kujenga Reli ya TAZARA, madaraja makubwa, Uwanja wa Mpira wa Benjamin Mkapa,
uwanja wa Ndege wa Zanzibar na Ujenzi wa Bomba la kusafirisha Gesi asilia
kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam.
Aidha akizungumzia Miradi ya Sekta ya Nishati, Makamba
alisema nchi hiyo imewezesha utekelezaji wa miradi zaidi ya 11, ikiwemo Ujenzi
wa kuimarisha Gridi ya Taifa kwa Ukanda wa Kaskazini na Mashariki, Ujenzi wa
Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP), Kituo
cha Kupoza na kupokea umeme cha Chalinze na maeneo mbalimbali nchini.
Makamba alitaja fursa zingine zilizopo katika sekta ya
nishati ambayo nchi ya china inaweza kuenndelea kushirikiana na Tanzania.
Fursa hizo ni pamoja na Kuimarisha Gridi ya Taifa, Utafutaji
na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi katika kina kirefu cha bahari, na Miradi ya
Usambazaji wa Umeme Vijijini.
Vilevile alieleza kuwa nchi hizo zibalishane wataalam ili
kujifunza zaidi, kuongeza ujuzi na ufanishi katika sekta husika, pia wafanye
utafiti ili kuibua miradi mipya itakayoweza kutekelezwa kwa ushirikiano wa nchi
hizo.
Pamoja na mambo mengine aliweka wazi matokeo chanya
yaliopatikana wakati wa ziara yake nchini China mwezi Juni mwaka huu kuwa ni
kuwepo kwa kampuni zaidi tisa ya pamoja na taasisi mbili zinazotaka kuja
kushirikiana na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati katika kuendeleza
miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati.
Na. Zuena Msuya- DSM
0 Maoni