Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema msimamo wa thabiti wa nchi ya Tanzania ni kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari, na ndio maana Serikali iliamua kufanya marekebisho ya Sheria ya Huduma ya Habari Sura ya 229, ili ikidhi uhuru wa vyombo vya habari.
Mhe. Nape amesema hayo jana jijini Dar es
Salaam alipokuwa akifungua Kozi Fupi ya 15 ya Wahariri wa Vyombo vya Habari
inayotolewa na Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
“Wanahabari niwahakikishieni msimamo thabiti wa nchi yetu ni
kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari. Mhe. Rais mara nyingi amekiwa akiagiza
kufanya kazi bila kuingilia uhuru wa Vyombo vya Habari,” amesema Mhe. Nape.
Aidha amewataka Wahariri hao mara watakapomaliza kozi hiyo
na kurudi katika vituo vyao vya kazi, wafanye kazi kwa kuangalia maslahi ya
nchi, vilevile amewataka kuendelea kulifanya Taifa kuwa kitu kimoja na kukuza
umoja wa Taifa.
Kwa upande wake Kansela wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Dkt.
Abdulhamid Yahya Mzee amesema kuwa mafunzo hayo kwa Wahariri wa Vyombo vya
Habari yataleta matokeo chanya kwa washiriki hao na kufanya Taifa lisonge
mbele.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Jenerali
Ibrahim Mhona ametaja kauli mbiu ya mafunzo hayo kuwa ni “Nafasi za Vyombo vua
Habari Katika Kuimarisha Usalama na Kukuza Umoja wa Kitaifa”.
“Kupitia kozi hii ya kimkakati, tunaenda kuona Wahariri
ambao wataenda kufanya kazi ya uhariri wa kimkakati kwa kizingatia maslahi ya
nchi yetu,” amesema Meja Jenerali Mhona.
Ametaja baadhi ya maeneo ambayo washiriki hao watafundishwa
kuwa ni, Dhana ya Usalama wa Taifa, Maslahi ya Nchi, Masuala ya TEHAMA na thari
zake pamoja na Wajibu wa Mhariri.
Na Lilian Lundo - WHMTH
0 Maoni