Mhe. Kigahe aitaka jamii kuwajengea watoto malezi yasiyo na hofu

 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, ameitaka jamii kuwajenga watoto malezi yasiyo na hofu wakati wa wa hatua za makuzi ili wawe raia wema na wenye kujiamini wanapokuwa wakubwa.

Kigahe ametoa rai hiyo alipotembelea Banda la Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika viwanja vya John Mwakangale kwenye maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayoendelea mkoani hapa.

"Ni ukweli kwamba, jamii ikiwajenga watoto katika kujiamini na kujisimamia katika wakati wa utoto wao utawawezesha kujiamini hata wanapokuwa watu wazima" amesema Kigahe.

Kigahe amepongeza juhudi zinazochujuliwa na Wizara hususan ni kukabiliana na vitendo vya ukatili na kusisitiza kwamba, jamii ikiwa na ukatili hata shughuli za uzalishaji Mali haziwezi kutendeka.

Awali Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Regina Molel amemuelezea Naibu Waziri huyo huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara hiyo ikiwepo huduma za msaada wa kisaikolojia, uwezeshaji wanawake kiuchumi na usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

"Sisi kama Wizara tunashiriki maonesho haya kwa mara pili mfululizo hivyo, tunajitahidi sana watu waelewe shughuli zetu ikiwepo usimamizi wa Taasisi zetu mbili na vyuo Nane vya Maendeleo ya Jamii " amesema Regina.

Mbali na Naibu Waziri kutembelea banda hilo la Wizara watu wengine waliotembelea ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini Mhe. Beno Malisa ambaye ameiomba Wizara kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa watembeleaji wa maonesho hayo.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ni moja ya Wizara inayoshiriki maonesho hayo ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani Mbeya.

Na WMJJWM Mbeya

Chapisha Maoni

0 Maoni