Mbwa mwitu kuongezeka zaidi Hifadhi ya Taifa Serengeti

 


Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imefanikisha zoezi la kuhamisha Mbwa mwitu wapatao ishirini (20) na kuwaachia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa lengo la kuendeleza shughuli za utalii na utafiti.

Akishuhudia zoezi hilo lililofanyika katika eneo la Makoma Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda B. Moronda amesema kuwa "zoezi hili ni la manufaa kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti kwani itasaidia kuongezeka kwa makundi ya wanyamapori na wageni kuweza kuwaona kwa urahisi".

"Mbwa mwitu hawa wakiongezeka itakuwa zao zuri la utalii, na watalii wataweza kufurahia na kushuhudia namna wanyamapori hawa wanavyowinda tofauti na ilivyozoeleka kuwaona Simba".

Aidha, amesisitiza kuwa wananchi pembezoni mwa hifadhi wasisite kutoa taarifa pale wanapowaona Mbwa mwitu hawa vijijini na sio kuwauwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha utafiti wa wanyama pori Serengeti (Tawiri) Dkt Emmanuel Masenga amesema viumbe hawa adimu wanatakiwa kuendelea kuwepo katika mfumo wa ikolojia, eneo ni salama na tunaongeza idadi yao ili tuweze kufikia malengo ya Uhifadhi.

Brigitha Kimario- Serengeti

Chapisha Maoni

0 Maoni