Amwagia maji ya moto mke mwenza kisa wivu wa mapenzi

 

Mwanamke Mariam Paul mwenye wa miaka 30 amejikuta katika wakati mgumu baada ya kummwagiwa maji ya moto na mke mwenzake ajulikaye kwa jina la Vumilia Kasomelo mwenye umri wa miaka 32 kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Inadaiwa kuwa Mariam Poul alienda katika kijiji cha Lugata kilichopo katika kisiwa cha Kome kuhudhuria msiba wa baba mkwe wake, ndipo akakutana na mke mwenzake huyo aliyepatwa na hasira na kummwagia maji ya moto usiku wa manane wakati alipokuwa amelala.

“Hadi sasa sijui shida ni nini hadi yeye kunimwagia maji ya moto mimi niko kwangu na yeye anaishi kwake tumekutana tu msibani kumzika baba mkwe wetu nashangaa yeye kuniunguza na maji ya moto,” amesema Mariam huku akiugulia machungu.

Ndagabwene Evarist mwenye umri wa miaka 33 ni mume wa wanawake hao amesema tukio hilo limemsikitisha sana kufuatia kutokea wakati wa msiba wa baba yake mzazi na kuiomba radhi jamii kwa tukio hilo na kudai wanawake hao hawajawahi kuonana siku hiyo ilikuwa ya kwanza ndipo tukio hilo likatokea.

“Nilikuwa nimechukua jukumu la kumuadhibu mke wangu mkubwa lakini jamii ikanizuia na kusema niache sheria itachukua mkondo wake” amesema Evarist.

Mwanamke anayedaiwa kufanya tukio hilo ambae ndiyo mke mkubwa Vumilia Kasomelo mwenye umri wa miaka 32 ambae ni mama wa watoto 6, alisema baada ya kumuona mke mwenzake alishikwa na hasira na kupelekea kufanya kitendo hicho cha kummwagia maji ya moto usiku alipokuwa amelala.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji kata ya Lugata Rafael Jangole amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa amekiri kutenda kosa hilo huku akisema kwamba kilichopelekea kufanya hivyo ni wivu wa mapenzi.

"Tunamshikilia kwa sasa huku tukiandaa taratibu za kumpeleka polisi kwa ajili ya taratibu zingine, Mariamu Paul ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake huku mkono wa kushoto ukiwa umeungua zaidi,” amesema Jangole.

Ndagabwene Evarist akiwa na mke wake mdogo Mariam Paul aliyemwagiwa maji ya moto na mke mkubwa Vumilia Kasomelo, ambaye anashikiliwa kwa kufanya kitendo hicho cha kikatili.

Chapisha Maoni

0 Maoni