Mapato ya NHC yapanda, yapanga kujenga nyumba nafuu 5000

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefanikiwa kuongeza mapato yake kutoka shilingi bilioni 144.42 mwaka 2021, hadi kufikia shilingi bilioni 257.47 mwaka 2022.

Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah Hamad, ameeleza hayo leo wakati akiongea na wahariri wa vyombo vya habari nchini kuelezea mafanikio ya shirika hilo.

Bw. Hamad amesema kwamba mwaka 20221/2022 mapato ya kodi ya NHC yamepanda na kufikia shilingi bilioni 90.76 kutoka shilingi bilioni 89.23 mnamo mwaka 2020/2021.

Pia, Bw. Hamad ameeleza kwamba mauzo ya nyumba yamepanda kutoka shilingi bilioni 29.33 mwaka 2020/2021 na kufikia shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/2022.

Ameongeza kwa kuwa faida halisi inayotokana na shughuli za shirika la NHC iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/2022 kutoka shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020.2021.

Bw. Hamad amesema kwamba kupitia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS), NHC inampango wa kujenga nyumba 5000 za gharama ya kati ambazo zitakuwa za kuuza na kupangisha.

“Asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa Dar es Salaam, katika Jiji la Dodoma asilimia 20 na katika mikoa mingine asilimia 30,” amesema Bw. Hamad.

Bw. Hamad ameongeza kwamba mradi huo wa SHS utakaotekelezwa kwa awamu utagharimu shilingi bilioni 466.

Chapisha Maoni

0 Maoni