WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma
kuwahudumia wananchi ipasavyo ili dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan ya kuendelea kutoa huduma bora na kwa wakati yatimie.
“Serikali haitaki mzaha, kama wewe ni muajiriwa wa Serikali
wewe ni mtumishi wa wananchi hivyo ni lazima uwahudumie. Watendaji nendeni
vijijini kwa wananchi na kusikiliza kero si vema wakasubiri hadi viongozi wa
kitaifa wanavyofika katika maeneo yao ndio watoe kero zao.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa michezo wa Majaliwa uliopo wilayani Tandahimba akiwa katika ziara ya
kikazi mkoani Mtwara.
Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali
kuwahudumia wananchi na kwamba Serikali iko makini katika kusimamia jambo hilo.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya
Tandahimba akamilishe taarifa ya uchunguzi wa mradi ya Kituo cha Afya cha
Mambamba ambapo Serikali ilitoa sh milioni 500 na bado ujenzi wake
haujakamilika.
Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema baada ya kukamilika kwa
taarifa hiyo apewe taarifa ya hatua zilichukuliwa kwa wahusika.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa huduma ya dawa katika
wilaya hiyo amesema Serikali inatoa shilingi milioni 77 kila mwezi, hivyo
hatarajii wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa
dawa. “Hakikisheni mnaleta dawa kulingana na magonjwa yanayowasumbua wakazi wa
Tandahimba.”
Pia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikagua na kuzindua mradi wa
maji wa kata ya Kitama wenye thamani ya shilingi milioni 797 na kutumia fursa
hiyo kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana kulinda vyanzo vya maji kwa
sababu vikiharibika watakosa huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprica
Mahundi amesema mbali na mradi huo pia Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa
maji wa Makonde wenye thamani ya shilingi bilioni 84 ambao utanufaisha wakazi
wa wilaya za Newala na Tandahimba, hivyo amewahakikishia wakazi upatikanaji wa
maji ya uhakika na salama.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni