Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila amewataka
wananchi kuzingatia ushauri wa afya unaotolewa na wataalamu ikiwemo kula kadri
inavyoshauriwa na wataalamu ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo
magonjwa ya Figo.
Mh. Chalamila ameyasema hayo leo wakati wa kuhitimishwa kwa
mbio za Figo Marathoni zilizofanyika leo katika viwanja vya mnazi mmoja kwa
lengo kukusanya fedha za kusaidia wahanga wa maradhi ya Figo ambazo
zimeratibiwa na MNH kwa kushirikiana na taasisi ya Healthier Kidney Foundation.
“Sisi tulio hai ndio tuna nafasi ya kusikiliza ushauri wa
kitaalamu na kuufanyia kazi kwa mustakabali wa afya zetu, huwa nikimsikiliza
Prof. Janabi anapotoa elimu naona kabisa vitu vingi anavyofundisha vinanigusa
kabisa, ni nafasi ya kila mmoja wetu kupanga kubadilika sasa kwa kuwa
tumeshasikia tatizo la Figo ni kubwa” amesema Mh. Chalamila.
Aidha, Mh. Chalamila mewataka wananchi kuwa na utaratibu wa
kukata bima za afya ili ziweze kuwafaa pindi wanapopata maradhi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amewataka wananchi kuwekeza katika afya kama
ambavyo wanawekeza kwa ajili ya kupata mafao ya uzeeni.
Amesema kuwa asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa wanaochuja damu
(Dialysis) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila)
wamepata maradhi ya Figo kutokana na changamoto ya shinikizo la juu la damu.
“Tafiti zinaonesha kuwa katika wanaume watano basi mmoja ana
shinikizo la juu la damu iwe ana jua au hajui, natoa wito kwa wananchi kuwa na
utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya kila mwaka na wanapobainika kuwa na
changamoto za shinikizo la juu la damu kutumia dawa kama inavyoshauriwa wa
wataalamu” amesema Prof. Janabi.
Naye, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Hospitali ya Taifa
Muhimbili Dkt. Jonathan Mngumi amesema kuwa maradhi ya Figo yanaongezeka kila
siku na kwamba asilimia 10 ya watu duniani sawa na watu milioni nane
wanachangamoto za maradhi ya Figo.
“Katika Kliniki ya Kuchuja damu Muhimbili Upanga tunahudumia
wagonjwa kati ya 90 hadi 120 wakati Mloganzila 30 hadi 50 kwa siku”.
Dkt. Mngumi ametaja sababu zinazosababisha maradhi ya Figo
kuwa ni matumizi holela ya dawa,
shinikizo la juu la damu na kisukari pamoja na tabia bwete.
Mwisho
0 Maoni