Sekta ya Madini nchini Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa
nchi nyingi za Afrika kwa namna ilivyoweza kurasimisha sekta ndogo ya uchimbaji
madini na hivyo kupelekea wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kupitia mfumo
ulio rasmi ambapo Serikali inaweza kufuatilia shughuli zao mpaka hatua ya kuuza
madini yao, kupitia katika masoko ya madini yaliyopo nchini.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman
Mwanga jijini Dodoma alipokutana na ujumbe kutoka Wizara ya
Madini na Maendeleo ya Migodi ya Jamhuri ya Zambia katika ziara inayolenga
kujifunza mifumo ya usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye shughuli za
uchimbaji wa madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo.
Dkt. Mwanga amesema kuwa, uwepo wa masoko ya madini
umewezesha wachimbaji kupata soko la uhakika pamoja na kuongeza mapato kutoka
Sekta ya Madini na mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika
mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2022 umefikia asilimia 9.1 ikiwa lengo ni
kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Naye, Meneja wa Biashara kutoka Tume ya Madini George
Kaseza, ameueleza ujumbe huo kuwa, hadi sasa kuna Masoko ya Madini 42 na Vituo
vya ununuzi wa madini 94 katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za uchimbaji
madini.
“Uwepo wa masoko ya madini umeongeza mapato kutoka shilingi
bilioni 8.30 Mwaka wa Fedha 2018/19 hadi kufikia shilingi bilioni 157.43 Mwaka
wa Fedha 2022/23,” amesema Kaseza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya
Madini Zambia Samson Phiri amesema mafunzo hayo nchini yamelenga kuwawezesha
wataalam wa Sekta ya Madini nchini Zambia kujifunza mifumo ya usimamizi wa
Sekta hiyo hususan kwenye shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanywa na
wachimbaji wadogo.
Ujumbe huo unatarajia kutembela Soko la Madini Mkoa wa
Shinyanga, Soko la Dhahabu mkoa wa Geita ili kujifunza namna biasharaya madini
inavyofanyika katika masoko hayo.
Ziara ya Zambia nchini inakuja ikiwa zimepita siku chache
tangu ujumbe kutoka nchi ya Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini na
Uchumi wa Bluu wa nchi hiyo Elijah Mwangi kufika nchini kujifunza kuhusu namna
bora ya usimamizi wa Sekta ya Madini.
#Hadi kufikia Desemba 2022 Serikali ya Tanzania imekusanya
jumla ya Shilingi bilioni 504.57 kutoka kwenye Masoko ya Madini tangu
yalipoanzishwa Machi 2019.
0 Maoni