WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji kutoka
kampuni nne za Urusi zenye nia ya kuwekeza nchini katika nyanja ya usindikaji
mazao, nishati jadidifu na utengenezaji wa vifungashio vya glasi.
Kampuni hizo ni SEIES (usindikaji mazao na mitambo yake),
Agrovent (kusindika mazao yanayoharibika haraka), Unigreen Energy (Nishati
Jadidifu) na TD Glass NN Expo LLC (utengenezaji wa chupa za vioo vya kutumia
mchanga na magadi).
Amekutana nao jana kwa nyakati
tofauti wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako
alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele
baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.
Akielezea kuhusu kampuni yao, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni
ya SEIES, Bw. Yuri Korobov amesema wanasindika vyakula kwa kukausha mazao bila
kuharibu viinilishe (nutrients) na vyakula hivyo vinaweza kuhifadhiwa kwa mwaka
mmoja.
“Tukianzisha mradi huu tunaweza kuhifadhi matunda na vyakula
vingi vilivyoko Tanzania. Tunatumia teknolojia ya kugandisha na kukausha maji
yote bila kuharibu viinilishe. Mradi huu unaweza kupanuliwa katika wilaya na
mikoa mingine nchini Tanzania kwani tumelenga wakulima walioungana kwenye vyama
vya ushirika,” amesema Korobov.
Bw. Korobov ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Kuratibu
Biashara za Taasisi za Umma nchini Urusi (Delovaya Rossiya) alisema wamepanga
kuwafundisha wafanyakazi ili wawe na elimu ya uhandisi wa kusindika mazao hayo.
Delovaya Rossiya ambayo pia ni maarufu kama “Business
Russia” ilianzishwa mwaka 2001, inaunganisha wafanyabiashara zaidi ya 7,000 na
ina uwakilishi kwenye majimbo yote 85 ya Shirikisho la Urusi.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Kampuni ya SEIES, Bw. Mikhail
Mikhailov alisema kampuni hiyo pia inabuni ufundi na kutengeneza vifaa
vinavyotumika kwenye teknolojia ya kukausha mazao. “Nchi zinazoongoza kwa
teknolojia hii ni China na Uturuki, tunaamini Tanzania inaweza kushindana nao na
kuwa mbele zaidi kwenye teknolojia hii.”
Kuhusu mitambo ya kukaushia mazao, alisema wanaweza kuunda
mitambo ambayo ikifika nchini inakuwa rahisi kuunganisha (assembling) na rahisi
kuijenga kwa haraka. “Mitambo yetu inaweza kusindika vyakula vya mafuta, vya
mimea, matunda, mbogamboga, maziwa, samaki na nyama.
Alilitaja eneo jingine wanaloweza kuanzisha ni utenegenezaji
wa friji zinazotumia nguvu ya jua badala ya umeme, na teknolojia ya kutengeneza
nishati ya umeme kwa kutumia takataka. “Hili ni suluhisho mara mbili kwani
tutapata umeme na kuhifadhi mazingira kwa kupunguza takataka,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya
Agrovent, Bw. Sergey Pribysh alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana nia ya kuja
kuwekeza Tanzania kwenye mazao yanayoharibika haraka kama vile maua na
mbogamboga.
“Kampuni yetu ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazozalisha
mitambo ya kusindika maziwa na nyama zinazotokana na ndege kama vile kuku na
bata. Tuko tayari kushirikiana na Watanzania na tumejipanga kutoa mafunzo ili
kuandaa wataalamu watakaoendesha mitambo hiyo. Itabidi tuwapate maafisa kilimo
ili wafundishwe jinsi mitambo inavyofanya kazi,” alisema Pribysh.
Naye Bw. Aleksey Tatarinov wa kampuni ya Unigreen Energy
alisema wana nia kuimarisha sekta ya nishati nchini kwani wana utaalamu wa
kutengeneza umeme jua na paneli zake, umeme wa upepo na wa jotoardhi
(geothermal).
Naye Mmiliki mwenza wa kampuni ya TD Glass NN Expo LLC, Bw.
Andropov Vasilyevich alisema wana kampuni inayotengeneza chupa za vioo vya
kutumia mchanga na magadi kwa hiyo wana nia ya kutengeneza ili wauze kwenye
viwanda vingine.
Waziri Mkuu amewahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji
kwani Serikali ya awamu ya sita imeweka msisitizo kwenye uwekezaji na maamuzi
yao ni sahihi kwa sababu Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza.
Amewaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania ina soko la uhakika
kwa kuwa inazungukwa na nchi za Kenya, Uganda, Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia,
Malawi na Msumbiji. “Unaweza kwenda kufanya biashara kokote.”
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea na mkakati wa
ujenzi wa miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kuchochea ukuaji wa
uchumi kupitia biashara na uwekezaji. “Tuna miundombinu ya reli, tuna barabara
nzuri karibu maeneo yote nchini, tuna ndege, tunayo maziwa makuu matatu
yanayowezesha usafirishaji wa bidhaa, pia malighafi tunazo za kutosha, kwa hiyo
karibuni sana Tanzania.”
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni