TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa
watatu 1. NAZARETH NDELE [50] 2. STEVEN MWAIGAGA [29] na 3. FARAJA MWAIGAGA
[26] wote wakazi wa Kijiji cha Igunda Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa tuhuma za
kumtorosha mwanafunzi na kutaka aolewe na kijana wao kinyume cha sheria.
Ni kwamba Juni 12, 2023 huko Kijiji cha Santilya, Mwanafunzi
wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Santilya (jina linahifadhiwa)
mwenye umri wa miaka 17 alikutana na CHANDE MWAIGAGA ambaye alimshawishi na
kuingia naye kwenye mahusiano ya kingono.
Julai 20, 2023 mtuhumiwa CHANDE MWAIGAGA alimfuata
mwanafunzi huyo kwenye makazi aliyokuwa amepangishiwa na baba yake mzazi
aitwaye MAJALIWA MISTON [46] Mkazi wa Kijiji cha Jojo – Mbalizi kutokana na
umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni na kisha kuondoka naye kwenda kuishi
naye kinyumba Kijiji cha Ilindi Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Julai 27, 2023 saa 3:00 asubuhi, MAJALIWA MISTON [46] akiwa
nyumbani kwake Kijiji cha Jojo alipokea ugeni wa watu watatu ambao ni NAZARETH
NDELE [50], STEVEN MWAIGAGA [29] na FARAJA MWAIGAGA [26] ambao walijitambulisha
kwake kuwa wao ni washenga wa CHANDE MWAIGAGA ambaye anaishi na binti yake na
kueleza lengo lao ni kutoa posa Tshs.110,000/=, Mahali Ng’ombe mmoja, Mbuzi
Jike mmoja, Blanket moja na mashuka mawili.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata
taarifa na kufika eneo la tukio na kutokana na ushirikiano na Mtendaji wa Kata,
Mwenyekiti wa Kijiji na Wananchi, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wote watatu ambao baadae waliowezesha kupatikana kwa binti huyo
akiwa nyumbani kwa mtuhumiwa. Jitihada za kumtafuta mtuhumiwa CHANDE MWAIGAGA
zinaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa vijana kuacha
tabia ya kuwalaghai na kuwarubuni wanafunzi kitendo ambacho ni kinyume cha
sheria na kinachosababisha kuwaharibia masomo. Aidha, Jeshi la Polisi linatoa
rai kwa wazazi/walezi kuacha kusaidia/kuungana na watoto wao katika vitendo vya
uhalifu.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.
0 Maoni