Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar, Bw.
Charles Hillary, ameonesha kukerwa na wachambuzi wa michezo pamoja na
watangazaji maarufu ambao wamekuwa wakikibananga Kiswahili katika vipindi mbalimbali
vya redio na televisheni wanavyotangaza kwa kuchanganya lugha.
Bw. Hillary ametoa kauli hiyo leo Zanzibar katika semina ya
Wahariri Wakuu wa Vyombo Vya Habari, iliyolenga namna bora ya kutumia Kiswahili
Sanifu katika Vyombo Habari, katika kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7.
“Kuna tatizo la kuchanganya lugha ya Kingereza na Kiswahili
haswa watu tunaowaita wachambuzi wa michezo, jambo hili sio zuri linakibananga
Kiswahili,” amesema Bw. Charles Hillary na kuongeza, “Watangazaji hawa hawana mswada
(script) inayowaongoza nini cha kuongea na mhariri wao hajui watachoongea, wao
wanajiongelea tu bila muongozo”.
Amesema kwamba kuna siku alikuwa anasikiliza kipindi kimoja
cha michezo cha redio na akawasikia wachambuzi wakitangaza kipindi kwa kuchanganya
lugha ya Kingereza na Kiswahili na akampigia Mhariri wao kumueleza tatizo hilo.
“Baada ya kumpigia Mhariri wao nikamwambia kama wanahamu sana
ya kuongea Kingereza wape dakika tano waongee lugha ya Kingereza wakimaliza waendelee
na Kiswahili, hawakufanya hivyo na nikasikia wanaongea Kiswahili tu nafikiri
Mhariri wao aliwaeleza,” amesema Bw. Hillary.
Ameongeza kwa kueleza kuwa hawa wachambuzi wa michezo huenda
wanachomekea maneno ya Kingereza kwa kujionyesha kwamba wao ni wataalamu sana
wa michezo katika kujikweza ili waonekane wanajua.
“Hakuna watangazaji wa kisasa ama wakizamani sisi vyombo vya
habari hatupaswi kukiharibu Kiswahili, wenzetu China ukiharibu lugha yao unafungwa,
si maanishi tufanye hivyo ila tunapaswa kukemea uharibifu wa Kiswahili,”
amesema Bw. Hillary, na kuongeza “Wamiliki wa vituo vya redio na televisheni
wamekuwa wakiajiri pia vijana maarufu sisi kwetu Zanzibar tunawaita chepechepe
hawa hawazingatii taratibu za utangazaji na hawajui maadili ya utangazaji”.
0 Maoni