Tume yapendekeza mabadiliko Jeshi la Magereza

Tume ya Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini Tanzania imependekeza Jeshi la Magereza kufanyiwa mabadiliko ya kimuundo ili lifanye kazi zake kwa ufanisi.

Hayo yamesemwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande, wakati akiwawasilisha Ripoti ya Tume ya Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Jaji Mkuu Mstaafu Chande amesema wamepokea taarifa za kuwapo kwa matumizi makubwa ya nguvu katika Jeshi la Magereza na kushauri jeshi hilo libadilishwe liwe sehemu ya kurekebisha tabia.

“Marekebisho hayo ya kimuundo yanapaswa kuwafanyia mafunzo askari magereza pamoja na magereza kuwa na shughuli za uzalishaji mali ili wafungwa wapate kujifunza kazi,” amesema Jaji Mstaafu Chande.

Ameeleza kwamba wamekutana na mfungwa mmoja ambaye yupo Dodoma kwa sasa ni fundi mzuri wa nguo na anawashonea nguo hadi viongozi, ambaye alijifunza gerezani kwa mfungwa mwenzake wa kutoka DRC.

Aidha, tume hiyo imependekeza magereza kuachana na matumizi ya kuni ambayo hutumika kuwapikia chakula cha wafungwa zaidi ya 31,000 nchini na kuchangia kuharibu mazingira.

“Tume inapendekeza magereza sasa kuacha kutumia kuni, na badala yake watumie nishati mbadala kama vile gesi, umeme na nishati nyingene rafiki kwa mazingira,” amesema Jaji Mstaafu Chande.

Kuhusu gharama kubwa za matibabu ya wafungwa nchini, Jaji Chande amesema kwamba tume inapendekeza kuwapo mpango wa kuwakatia wafungwa bima ya makundi ili kupunguza gharama hizo.

Chapisha Maoni

0 Maoni