Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali vijana na
itaendelea kulinda maslahi yao wakati wote.
Pia, Mheshimiwa Katambi ametoa wito kwa vijana nchini
kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali kupitia programu za kuwawezesha na
miradi mikubwa ya kimkakati ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutatua
changamoto ya ajira miongoni mwa vijana.
Mhe. Katambi ameyasema hayo leo Julai 8, 2023 wakati
akifungua bonanza la michezo la vijana wa mradi wa USAID KIJANA NAHODHA
unaotekelezwa na Shirika la T-MARC Tanzania, ambalo limefanyika katika uwanja
wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Amesema kuwa, Serikali imedhamiria kuwajengea vijana uwezo wa
masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, utamaduni na kiafya ili kuwa na
nguvukazi imara.
“Michezo ni afya na michezo ni maisha, hivyo niwahamasishe
vijana kuchangamkia fursa hii ili kuimarisha afya zenu kimwili na kiakili kwa
kujenga taifa lenye nguvu kazi ya vijana walio imara na pia kutumia michezo hii
kama chanzo cha ajira,” amesema
Vile vile, Naibu Waziri Katambi amesema Mradi huo wa USAID
Kijana Nahodha ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na serikali kwa
kushirikiana na mataifa na wadau wa maendeleo nchini katika kuimarisha ustawi
na maendeleo ya vijana kiuchumi na kijamii.
Akizungumza awali, Mkurugenzi wa mradi huo, Dkt. Tuhuma
Tulli, amesema mradi huo unafadhiliwa na USAID na unalenga kusaidia vijana
wenye umri wa miaka 15 hadi 25 hususan walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa
kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi, ujuzi, ujasiriamali, kilimo, masuala ya
afya, uraia na uongozi.
“Bonanza hili ni sehemu ya kuhamasisha vijana wetu
kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazo wainua kiuchumi na kuwafanya kuwa raia
bora wa taifa lao na viongozi bora baadae,” amesema Tulli.
0 Maoni