Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea
kutekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa afya ya mama
na mtoto ikiwemo mpango wa Mama Samia Mentorship Program.
Amesema kuwa mpango huo ni mahsusi kwa mafunzo ya muda mfupi
kazini kwa madaktari bingwa na wakunga ili waweze kuimarisha utoaji huduma
kwenye Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.
Amesema hayo leo (Jumapili, Julai 23, 2023) aliposhiriki
katika mbio za NBC ‘NBC Marathon’ zilizofanyika jijini Dodoma.
Mh. Majaliwa amesema kuwa mpango mwingine wa Serikali ni
kuongeza wigo wa kutoa huduma za kupima dalili za awali za saratani ya uzazi
kutoka Vituo vya Afya 925 vilivyopo hadi kufikia vituo vya Afya 1,025 hapa
nchini.
“Mwingine ni kuimarisha wigo wa kutoa huduma za watoto
wachanga kwa ujenzi wa wodi maalum, kununua vifaa tiba na mafunzo kwa watumishi
kutoka hospitali 175 hadi kufikia hospitali 275 katika mwaka 2023/2024”.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na sekta binafsi zenye lengo la kuinua
michezo kama wanavyofanya NBC.
“Suala hili lipewe kipaumbele kwani sote tunatambua kuwa
michezo ni zaidi ya burudani na inachangia ajira na huduma za afya nchini,”
alisema Mh. Majaliwa.
Mbio za NBC kwa mwaka 2023 zinatarajia kukusanya Sh. milioni
300 ambazo zitatumika kuboresha afya ya mama na mtoto, kusaidia mapambano dhidi
ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa
taaluma ya ukunga nchini ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi.
Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt.
Pindi Chana amesema kuwa michezo ni nyenzo ya mabadiliko kwa jamii katika
kuelimisha, kuimarisha afya na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
“Tutaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi na
milango ya wizara ipo wazi. Lengo ni kupunguza wagonjwa wanaolazwa hospitali
kwa kuhamasisha Watanzania kushiriki kwenye michezo ili kukabiliana na magonjwa
yasiyoambukiza,” alisema Dkt. Chana.
Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni