Serikali imejipanga kutumia tafiti mbalimbali zinazofanyika
kwa lengo la kuwa na afua na mikakati itakayosaidia kuondokana na vitendo vya
ukatili hasusan dhidi ya Watoto na Vijana nchini.
Hayo yamebainika jijini Dodoma Julai 24, 2023 katika kikao
kazi cha kujadili utafiti kuhusu Ustawi, Afya ya Watoto na vijana
kilichowakutanisha Makatibu wakuu kutoka Wizara za kisekta Tanzania Bara na
Zanzibar.
Akiongoza kikaokazi hicho Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju
amesema, kikaokazi hicho kimelenga kuangalia namna bora ya kuwa na mikakati ya
kufanya tafiti itakayo saidia kutatua suala la ukatili na mmonyoko wa maadili
nchini.
Mpanju amesema utafiti huo ni muhimu kwa mstakabali wa
Ustawi wa Watoto na Vijana wa kitanzania na ni nyezo muhimu ili kuhakikisha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inaweka mifumo mizuri ya ulinzi na usalama wa watoto na vijana.
"Tumeamua kufanya utafiti huu ili iweze kutupa matokeo
na kutusaidia kupata afua za kupambana na ukatili dhidi ya ukatili wa watoto na
vijana katika jamii hasa kupata viwango aina na madhara ya ukatili ndani
hamii" alisema Wakili Mpanju
Amesisitiza kuwa utafiti huo itasaidia kung'amua masuala
mbalimbali ambayo yamechangia uwepo wa ukatili ili kisaidia Serikali zote mbili
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na
afua nzuri za kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Akieleza mikakati mbalimbali ya Serikali katika kupambana na
ukatili nchini ni uwepo wa Mpango wa Kitaifa wa kupambana na Ukatili dhidi ya
Wanawake na Watoto, Madawati ya Jinsia katika Jeshi la Polisi, Magereza,
Taasisi za Serikali, maeneo ya umma, Madawati ya Watoto Shuleni na mikakati
mbalimbali ya kupambana na tatizo hilo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Zanzibar Siti Abbas Ali
akitoa maelezo wakati wa kikao kazi amesema utafiti huo utasaidia pia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar kuwa na afua mbalimbali
zitakazosaidia Serikali kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii hasa
kwa watoto na vijana vinavyoathiri kundi hilo ambalo ni muhimu katika Ustawi wa
Taifa lolote duniani.
Akiwasilisha muhtasari wa utafiti tarajiwa wakati wa kikao
kazi hicho Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS)
Dkt. Redemta Mbatia amesema kuwa utafiti wa UNICEF kuhusu masuala ya ukatili
unaonesha kuwa watoto Billioni 1 kati ya umri wa miaka 2-17 walikuwa
wamefanyiwa ukatili wa kimwili kingono na kisaikolojia katika Kipindi cha mwaka
mmoja 2022 hivyo ni muhimu kufanya utafiti utakaosaidia kupata mikakati
mbalimbali ya kupambana na vitendo hivyo katika jamii.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshugulikia na masuala ya watoto (UNICEF) John George amesema wataendelea
kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha utafiti huo unafanikiwa ili
kuwezesha kufanya shughuli zao hasa katika kupambana na ukatili dhidi ya Watoto
Duniani hasa katika kuweka Mipango, Sera, Miongozo na Sheria za kumlinda dhidi
ya vitendo vya ukatili.
"Na sisi kama Shirika utafiti huo utatusaidia kupata
taarifa ambazo zitatuwezesha kuweka Mipango na mikakati katika kutekeleza
shughuli mbalimbali zinazohusu afua za watoto hasa katika kupambana na vitendo
vya ukatili hasa dhidi ya watoto " alisema John.
Akichangia katika kikaokazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya
Katiba na Sheria Mary Makondo amesema ni muhimu kuangalia pili upande wa kesi
za ukatili dhidi ya Watoto na namna gani Taasisi mbalimbali za Serikali na
wadau watashirikiana katika kuhakikisha kesi za ukatili zinasimamiwa vyema na
kuhakikisha wahanga wa vitendo hivyo wanalindwa na watuhumiwa wanafikishwa
katika vyombo vya Sheria.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa Kitaifa na kimataifa
wanashirikiana katika kufanya utafiti kuhusu Ustawi, Afya ya Watoto na vijana
utakaosaidia kutatua changamoto za vitendo vya ukatili hasa dhidi ya Watoto na
Vijana.
Na. WMJJWM Dodoma
0 Maoni