Watalii wanaotembelea vivutio vya Utalii nchini hususan eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wameendelea kuvutiwa na aina mbalimbali za shughuli za utalii zilizoko katika Hifadhi hiyo.
Shughuli za utalii ambazo zinafanyika katika hifadhi ya
Ngorongoro ni pamoja na utalii wa picha (Photographic tourism), utalii wa
kutembea (walking safaris), Utalii wa akiolojia (archeological tourism) katika
Bonde la Olduvai na Laetoli, utalii wa kupanda maputo angani (hot air balloon)
na utalii wa kupanda milima (Mountain hiking) ambayo vyote vinapatikana katika
hifadhi ya Ngorongoro.
Bw. Remen Rudolff kutoka Marekani ameelezea kufurahishwa na
utalii wa picha katika bonde la Ngorongoro lenye umbo la kipekee la mandhari
asilia yaliyopambwa na mtawanyiko wa wanyama na ndege mbalimbali.
“Niko katika eneo zuri na la kipekee duniani ambalo kila mtu
anapaswa kuwa na ndoto ya kufika hapa, tumekuwa na muda mzuri wa kutalii,
waongoza utalii wetu ni wakarimu sana na wajuzi wa hadithi za porini na tabia
za wanyamapori, tumeona vivutio vingi; wanyama, mimea, ndege na maeneo ya
malikale ambavyo kwa ujumla vinaipa Ngorongoro uzuri wa kipekee kwa Afrika na
duniani kwa ujumla,” alisema Bw. Rudolff.
Kwa upande wake Sarah Tery kutoka Canada anabainisha kuwa
yeye kama mpenda utalii wa kutembea amefurahi utalii wa matembezi (walking safari)
akiwa Ngorongoro hasa katika eneo la Endoro ambapo wakiwa matembezi na wenzake
katika eneo la Endoro ameona tembo na nyati na kuona msitu uliotunzwa vizuri,
maporomoko ya maji ya endoro, kusikika kwa sauti za ndege wazuri wakiwa katika
mazingira asilia na kushuhudia mapango ya tembo (Elephant caves) ambayo tembo
huchimba kama sehemu ya kuja kupumzika na kulamba udongo ambao ni sehemu ya
virutubisho katika miili yao.
Baadhi ya watalii hupendelea utalii wa kutembea kwa miguu
katika vivutio vilivyopo upande wa Kaskazini mashariki mwa hifadhi Ngorongoro
ambavyo ni Kreta ya Empakai, Kreta ya Olmoti na Mlima Lolmalasin ambao ndio
mlima wa tatu kwa urefu nchini Tanzania ukiwa na urefu wa Mita 3,666.
Watalii wanaopenda utalii wa akiolojia na mambo kale wamekuwa
wakitembelea eneo la Bonde la Olduvai lenye utajiri wa gunduzi mbalimbali
ikiwemo fuvu la binadamu wa kale Zinjanthropus, Makumbusho Hai ya Dkt. Mary
Leakey, mchanga unaohama pamoja na Nyayo za Laetoli zenye umri wa miaka
takriban Milioni 3.6 iliyopita.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Freddy Manongi
kati ya mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 jumla ya watalii 752,232 walitembelea
eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, hii ni tofauti na mwaka wa fedha 2021/2022
ambapo jumla ya watalii walikuwa 425,386.
Na Kassim Nyaki, Ngorongoro.
0 Maoni