Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwa mara ya kwanza Maadhimisho ya siku ya Mwaka mpya wa Kiislamu; Mwaka 1445 Hijriya kutambuliwa na Serikali kuwa ni siku ya mapumziko.
Serikali imekubali ombi la Waislamu kuhusu kuiadhimisha siku
hii na kuwa ya mapumziko kwa madhumuni ya kuipa hadhi na kuiongezea hamasa siku
ya mwaka mpya wa Kiislamu kila inapofika.
Ameyasema hayo leo katika hafla ya Maadhimisho ya
kuukaribisha kuingia mwaka mpya wa Kiislamu yaliyofanyika Msikiti wa Munawar
Mfikiwa, Wilaya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kwa Mamlaka ya kikatiba chini ya kifungu 6(1)(a) cha Sheria
ya Masuala ya Rais wa Zanzibar, Namba:3 ya 2020, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitangaza rasmi kesho
Jumatano itakuwa ni siku ya mapumziko Kitaifa Zanzibar.
Aidha, Rais Alhajj Dk. Mwinyi ametoa wito kwa Wazazi na
Walezi kutimiza wajibu wa malezi ya vijana kuwa na kizazi chema chenye kumjua
Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza maarimsho yake na kujiepusha na makatazo katika
misingi bora ya maadili kwa mujibu silka na tamaduni za dini.
Vilevile, kuwa raia wema na wazalendo wa kuijenga nchi kwa
kuendelea kudumisha amani iliyopo kwa kila mmoja.
0 Maoni