WAZIRI MKUU Mh. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Urusi
imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwemo Tanzania.
“Mwelekeo wa mkutano wa leo ilikuwa ni kuona namna gani
tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Urusi. Wao wametoa
mwelekeo wa namna ambavyo wataweza kushirikiana na nchi za Afrika kuboresha
uchumi wa kila nchi na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye nchi yetu
ambao Rais Putin ameuridhia,” alieleza Mh. Majaliwa.
Ameyasema hayo jana baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili
wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi
ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo umefanyika
kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg,
Urusi. Akizungumza
Waziri Mkuu amesema Tanzania itaendelea kuimarisha
miundombinu ya usafirishaji kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa
kutumia rasilmali zake ikiwemo madini, maliasili na kilimo hasa upatikanaji wa
mbolea. “Tumesisitiza pia matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya
kuwawezesha wananchi wa vijijini ili nao wamudu kutumia nishati mbadala kukuza
uchumi wao,” amesema.
Amelitaja eneo jingine kuwa ni kukuza biashara ya mazao
baina ya Afrika na Urusi ambapo yenyewe inaweza kuwa soko la moja kwa moja ama
kwa kuwatumia marafiki zake. “Ili kufikia hayo, jitihada za kila nchi kwenye
kilimo zimesisitizwa. Tanzania tumeeleza mkakati wa kukuza kilimo ikiwemo
umwagiliaji. Pia tunahitaji mbolea, madawa na vitendea kazi ili tufanikiwe kwa
kasi zaidi.”
Waziri Mkuu Mh. Majaliwa aliwaeleza viongozi hao wa Afrika
juu ya Mkakati wa Rais Dkt Samia wa kutoa elimu bure na vifaa vya kufundishia kwa
lengo la kuwapunguzia mzigo wazazi.
Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Urusi, Vladmiri Putin
alisema nchi za Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Urusi
na kwamba nchi hiyo imekuwa ikiendelea kutoa misaada bila vikwazo kwenye maeneo
mbalimbali.
Akitoa mfano, Rais Putin amesema nchi 40 kutoka Afrika
zimenufaika na misaada ya kijeshi ikiwemo mafunzo. “Ukaribu wa mahusiano kati
ya Afrika na Urusi unazidi kuongezeka. Tunatarajia kufungua balozi zetu kwenye
nchi nyingine kama vile Burkina Faso na Equatorial Guinea. Pia tunatarajia
kufufua vituo vya utamaduni vya Kirusi. Hivi sasa, vituo kama hivyo vinafanya
kazi kwenye nchi nane tu,” alisema.
Alisema nchi hiyo itaendelea kutoa misaada kwenye sekta ya
kilimo ili kuimarisha upatikanaji wa chakula. “Jana ndiyo maana nilitoa ahadi
ya kuzipatia nafaka nchi sita tani kati ya 25,000 hadi 50,000 na kwamba
zitasafirishwa bure”.
Nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Zimbabwe, Jamhuri ya Kati,
Eritrea na Somalia. Alisema Urusi imepanga kutoa dola za Marekani milioni 90
kwa nchi za Afrika kulingana na maombi ambayo yamepokelewa kutoka Umoja wa
Afrika (AU).
0 Maoni