Nyumba ya Mama Ngina Kenyatta yaondolewa polisi yalindwa na walinzi binafsi

 

Nyumba ya mke wa aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa la Kenya Hayati Jomo Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta iliyopo Muthaiga inalindwa na walinzi wa kampuni binafsi baada ya serikali kumuondolea walinzi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na gazeti la Nation, walinzi wa Mama Ngina waliondolewa jumanne usiku, baada ya ofisi za GSU na Polisi wa Utawala kuwaagiza kuondoka na kuripoti kwenye kituo cha polisi.

Kuondolewa kwa walinzi hao, kumekuja baada ya Rais William Ruto kudai kwenye mkutano wake huko Naivasha kuwa aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, anawafadhili wapinzani kufanya maandamano ya kuipinga Serikali.

Mama Ngina, mama wa Uhuru Kenyatta alikuwa anapatiwa ulinzi wa askari polisi 30 kulinda nyumba yake hiyo yote, kabla ya kupunguziwa na kubakia polisi wanane mwaka 2022, na sasa ameondolewa polisi wote.

Chapisha Maoni

0 Maoni