Makumbusho ya Taifa la Tanzania itaendelea kushirikisha
jamii na wadau katika wajibu wa kuhifadhi Urithi wa asili na utamaduni wa
Tanzania kwa kuweka uwiano sawa wa jamii kuifikia Makumbusho kwa kushirikisha
makundi mbalimbali yakiwemo ya Watoto wenye uhitaji maalum katika program
zitakazoisogeza jamii karibu zaidi na Makumbusho.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya
Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utamaduni
wa Mtanzania na Ujerumani yaliyofanyika Kijiji cha Makumbusho kilichopo
Kijitonyama jijini Dar es Salaam yaliyohudhuriwa na vijana kutoka nchini
Ujerumani na Watoto wenye uhitaji maalum kutoka eneo la Manzese jijini Dar es
salaam wanaofadhiliwa na taasisi ya Youth Crossing Boundaries Foundation.
Dkt.Lwoga amesema kupitia matukio haya jamii inaweza
kujifunza na kubadilishana uzoefu wa tamaduni mbalimbali na hatimaye kujenga
uelewa wa pamoja wa tofauti za tamaduni na hatimaye kuleta amani katika jamii
hususan kwa watoto wenye uhitaji maalum ambao aghalabu hukosa fursa ya
kujifunza masuala mbalimbali.
Kwa upande wake Mwanzilishi wa Taasisi ya Youth Crossing
Boundaries, Father. George Rupperecht kutoka nchini Ujerumani amesema lengo ni
kuwapatia haki ya elimu Watoto wenye uhitaji maalum kuanzia ngazi ya elimu ya
msingi mpaka vyuo vikuu.
Amesema kuwa kupitia tukio hili katika Makumbusho ya Taifa
Watoto wataweza kujifunza utamaduni wao na kupata uzoefu wa tamaduni zingine
ili kukuza uelewa wao kuhusu masuala ya Utamaduni.
0 Maoni