Chongolo aitaka Serikali kuendelea na maboresho ya bandari ya Dar es Salaam

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema chama hicho kitaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha utendaji wa bandari zote za Tanzania kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya CCM.

Akizungumza jana Jijini Mbeya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Daniel Chongolo, amesema kwamba miradi yote inayotekelezwa na serikali imetokana na misingi ya CCM kutokana na kile wanachokiamini ili kuleta maendeleo ya taifa.

Ndugu Chongolo amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa makini katika utekelezaji wa Ilani kwa kuzingatia ahadi za maendeleo ambazo wamekuwa wakitoa zikiwemo za ujenzi wa barabara.

Katika mkutano huo Ndugu Chongolo amesema, “Bandari zote zitafanyiwa maboresho ikiwemo ya mkoa wa Tanga, Mtwara pamoja Dar es Salaam kutokana na kuwa jambo hilo lipo kwenye Ilani ya CCM”.

Amesema kuwa CCM ina malengo na mipango katika kuhakikisha wanapiga hatua katika kuwaletea maendeleo watanzania, na kuitaka Serikali kuendelea na mchakato wa awamu ya pili katika makubaliano ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni