Dkt. Abbasi, Balozi Ireland Wazindua Msafara Kinubi Mlima Kilimanjaro

 


Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amemwakilisha Waziri wa sekta hizo Mhe. Mohamed Mchengerwa kuwaaga wasanii kutoka nchini Ireland wanaokwenda kilele cha Mlima Kilimanjaro kuweka rekodi ya dunia ya Guinness.

Akiwa na Balozi wa Ireland nchini, Mary O’Neil, Dkt. Abbasi amewasilisha pia salaam na baraka za Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisema tukio hilo limepewa heshima kubwa kwa kuona umuhimu wake katika kutangaza utalii kama alivyofanya Rais Samia katika Royal Tour.

“Mna baraka zote na tumewaombea hata kwa mababu mfike salama kileleni ili dunia nzima ijue kwamba juu ya Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania rekodi ya dunia imewekwa kwa mtu kutoka Iteland kufanya Tamasha kubwa la kupiga kinubi,” alisema Dkt. Abbasi.

Balozi wa Ireland nchini Mhe. O’Neill anasema kinubi na nyimbo zitakazoimbwa kileleni ni vitu ambavyo ni sehemu ya utamaduni wa Ireland na kwamba mamilioni ya watu wa nchi hiyo watafuatilia tukio hilo mbashara.

Kwa upande wake msanii kiongozi kutoka nchini Ireland atakayeongoza wenzake takribani 20 katika Tamasha hilo kileleni, Siobhan Brady, anasema alipoweka rekodi ya Guinness juu ya kilele cha Mlima Himalaya India kwenye futi 16,000 mwaka 2018, alidhamiria kuja Mlima Kilimanjaro kuvunja rekodi hiyo kwa kukwea futi 19,000.

Dkt. Abbasi na Balozi O’Neill pia wamezipongeza kampuni za Mauly Tours ya hapa nchini na Worldwide Adventure ya Ireland kwa kuratibu tukio hilo na kuwasisitiza makampuni mengine ya utalii yanapopata wageni mashuhuri kushirikiana na Serikali katika kuyatangaza matukio hayo kwa faida ya utalii wa Tanzania.

Jumla ya watu 92 wameanza safari hiyo ya kuelekea kileleni leo Julai 20, 2023 wakiwemo waandaaji wa tamasha hilo pamoja na waongoza wageni.

Na Mwandishi Wetu, Machame, Kilimanjaro

Chapisha Maoni

0 Maoni