Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali wasiwe kikwazo waendelee kutoa
ushirikiano viongozi wa dini na wawekezaji wa ndani na nje ili waweze
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amesema
Serikali itaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji na kushirikiana na
sekta binafsi pamoja na madhehebu yote ya dini katika kutekeleza majukumu
mbalimbali.
“Katika hili
nasisitiza watendaji wote wa Serikali kuendelea kuziunga mkono taasisi binafsi
zinazotoa huduma kwa wananchi ili ziweze kutimiza malengo yake.”
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 20, 2023) katika sherehe za Maadhimisho ya
Miaka 40 ya cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini Arusha.
Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kumpongeza Askofu Mkuu wa Makanisa ya International
Evangelism na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Eliud Issangya kwa kuongoza vema chuo
hiko ambacho kimetimiza miaka 40.
“Nimefurahi
sana kusikia idadi ya wahitimu wa chuo hiki imefikia zaidi ya 10,000 ama kwa
hakika mmeweza kuweka hazina kubwa ya watendaji katika shamba la Mungu.”
Akizungumzia
changamoto mbalimbali zinakikabili chuo hicho ikiwemo ya barabara, Waziri Mkuu
ameuagiza uongozi wa TARURA mkoani Arusha kuhakikisha barabara hiyo ya kutoka
Kikatiti hadi Sakila inakarabatiwa.
Naye, Dkt.
Issangya amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha
maridhiano na kuwatua moyo viongozi wa dini, hivyo kuwawezesha kutekeleaza
majukumu yao kwa urahisi.
Amesema
uimara wa Serikali umewawezesha viongozi wa dini zote nchini kupendana, kufanya
kazi kwa kushirikiana, kuaminiana na kuheshimiana.
Kwa upande
wake, Askofu wa Kanisa la International Evangelism la nchini Congo, Askofu
Byamungu Magala ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu.
“Tanzania ni
Taifa ambalo limejaa amani na utulivu na ni Taifa ambalo halina ubaguzi wa dini
wala kabila, Taifa zuri linalopokea wageni bila ya shida yoyote. Nawapongeza
viongozi wa Taifa hili.”
Amesema
nchini kwao kuna matatizo hawana utulivu, hivyo hawawezezi kumuamudu Mwenyezi
Mungu kwa amani kama ilivyo Tanzania.
“Kila
ninapokuja hapa namuomba Mungu nasi atupe amani. Amani hii mliyonayo mnatakiwa
kuilinda kwa sababu Taifa bila amani raia watakuwa na matatizo makubwa, sisi
watu wanauawa kinyama.”
Pia,
amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri na kumtuma
Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhudhuria sherehe hizo. “Hali hii inaonesha namna
ambavyo viongozi wa Serikali wako karibu na raia na wanyenyekevu sana tofauti
na kwetu.”
CHANZO: Ofisi
ya Waziri Mkuu
0 Maoni