Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa, Mohamed
Mchengerwa amesema kuongezeka kwa idadi ya watalii kitaifa kumevunja rekodi ya
mapato katika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya
Maliasili na Utalii katika Bunge la 12, mkutano wa 11 kikao cha 39 jijini
Dodoma hivi leo.
“ Taasisi za utalii
nchini zimevunja rekodi ya mapato katika maeneo yao mfano TANAPA kwa mwaka
mzima wa 2021/22 walikusanya TZS bilioni 174, kwa miezi 10 tu ya mwaka huu wa
fedha, wameshakusanya TZS Bilioni 291 mapato haya kwa taasisi ni makubwa kuliko
yoyote yaliyowahi kukusanywa tangu zianzishwe.”
Aidha, mapato haya yametokana na juhudi zilizofanyika za
pamoja kutangaza vivutio vya utalii na kuimarika kwa miundombinu ya utalii
ndani ya hifadhi.
Aliongeza kuwa Shirika litaendelea na juhudi zote kuimarisha
shughuli zake za ulinzi, ikolojia, kutangaza utalii, kukusanya maduhuli na
kuimarisha miundombinu ili tuendelee kuvunja rekodi na watalii kufurika zaidi
katika hifadhi zetu.
“ Shirika litaendelea kuboresha miundombinu ya huduma za
utalii kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 500 na kukarabati
kilometa 10,500. Vilevile shirika litakarabati kilomita 300 za njia ya miguu za
kupanda milimani; kujenga mifumo ya usambazaji wa maji safi na malango 10 ya
kukusanya mapato katika hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa (1), Serengeti (2),
Kilimanjaro (1), Tarangire (1), Ruaha (1), Katavi (1), Nyerere (1), na Mikumi
(2).
Pia, Shirika litajenga studio ya kurusha vivutio vya utalii
mubashara utakaowezesha vivutio kurushwa moja kwa moja kwenye mitandao na
chaneli za kimataifa.”
Wizara ya Maliasili na Utalii leo imewasilisha makadirio ya
Bajeti ya jumla ya Shilingi 654,668,208,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024
matumizi ya fungu 69 kwa mwaka wa fedha. Kati ya fedha hizo TZS 486,501,449,000
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na TZS 168,166,759,000 ni za miradi ya
maendeleo.
Na. Brigitha Kimario - DODOMA
0 Maoni