Wanavijiji wa vijiji vinne vya Mpapayu, Tanganyika, Mlingano
na Kwalubuye wilayani Muheza mkoani Tanga wamekuwa wakiishi kwa hofu kufuatia
uwepo wa simba wawili walioingia Muheza kutokea Masaika, ambao wamekuwa wakila
mifugo yao usiku.
Taarifa ya Afisa Maliasili Muheza, Obadia Msemo, imeeleza
kuwa tarehe 28 na 29 kwa upande wa Masaika unaopakana na Muheza simba hao walikula
punda mmoja na mbuzi mmoja, na tarehe 30 walibainika kuwepo upande wa Muheza
baada ya kuonekana kwa nyayo zao.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba tarehe 30 kuamkia tarehe
31 katika kijiji cha Mpapayu aliliwa punda mmoja, jana tarehe 01.06.2023 majira
ya asubuhi nyayo za simba zilionekana katika kijiji cha Tanganyika kata ya
Lusanga, ambapo baadaye jioni walipokea taarifa za uwepo wao kitongoji cha Kizota
kijiji cha Mlingano.
Pia usiku wa kuamkia leo tarehe 02 kitongoji cha Mshukuruni
kijiji cha Kwalubuye Mwenyekiti wa Kijiji hicho ameripoti kuwa usiku ng'ombe
mmoja ameliwa. “Hivyo, Hali bado si salama kwa kuwa TAWA hawajafanikiwa
kukutana na simba, pia mashambulizi yao yamekuwa ya wakati wa usiku”.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya Muheza amesisitiza wanavijiji
kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki, wakati huu ambapo wataalamu
wa wanyamapori kutoka TAWA waliopo Muheza na wengine wanaotegemewa kutoka TAWIRI,
wakiwasaka simba hao.
0 Maoni