Halmashauri zaongoza kwa ukiukaji wa maadili

 

Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi, ameeleza kwamba kwa sasa halmashauri ndio zimekuwa zikiongoza kwa kuwa na malalamiko mengi ya vitendo vya ukiukaji wa maadali.

Jaji Mwangesi amesema hayo leo Dar es Salaam, wakati akiongea katika mkutano na Wahariri wa vyombo vya habari nchini, na kuongeza kwamba bado kunatatizo la uadilifu katika baadhi ya viongozi wa umma nchini.

“Bado kuna changamoto ya uadilifu kwa viongozi wa umma hivyo basi jamii ikiwamo waandishi wa habari wanapaswa kusaidia katika kuibua vitendo vya ukiukwaji wa maadili nchini,” alisema Jaji Mwengesi na kuongeza, “Sisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni wachache, hivyo basi ni muhimu wadau wote kushirikiana katika kuibua vitendo vya ukiukwaji wa maadili”.

Akijibu swali la kuvuliwa ubunge mbunge mmoja na Spika wa Bunge lililopita wakati Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ikijua kwamba mbunge huyo anaumwa na alikuwa akipatiwa matibabu nchini Ubelgiji, Jaji Mwengesi alisema kwamba wao hawana mkono katika suala hilo.

“Sisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hatuna mkono katika kuvuliwa ubunge mbunge huyo, utaratibu ni wabunge wakijaza fomu za matamko ya Rasilimali, Maslahi na Madeni kwa Spika kwanza,” alifafanua Jaji Mwengesi na kuongeza bila kutaja jina la mbunge huyo, “Hivyo kilichofanyika ni kwa Spika kuchukua maamuzi hayo kutokana na kutokuwa na fomu za tamko la mbunge huyo, ila sisi hatukuhusika kabisa katika suala hilo”.

Juni 28, 2019 aliyekuwa Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, alitangaza kiti cha ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa kinashikiliwa na Tundu Lissu (CHADEMA) kuwa wazi, kwa sababu za utoro bungeni pamoja na kutojaza Tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni. 

Akiongelea kuhusiana na kufanyika kwa utafiti juu ya hali ya maadili nchini, Wakili wa Serikali Mkuu/Mkuu wa Kitengo cha Sheria Bi. Emma Gelani, amesema mara ya mwisho kufanya utafiti ilikuwa mwaka 2016, ambapo hali ya uadilifu ilionyesha kuwa ni juu ya asilimia 50.

“Utafiti wa mwaka 2016 hali ya uadilifu ilikuwa nzuri ilikuwa juu ya asilimia 50, ila kwa sasa hatujafanya utafiti tangu mwaka huo japo kwa sasa ipo haja lakini tumekuwa hatuna fungu la fedha za kufanya utafiti huo,” alisema Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Gelani.

Chapisha Maoni

0 Maoni